Wadau wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya UKIMWI katika Halmashauri ya Mji Njombe wamekutana kwa lengo la kujadili utekelezaji wa shughuli zinazofanywa kwenye mapambano na changamoto zinazowakabili.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau Mwenyekiti wa Kamati ya kudhibiti UKIMWI Halmashauri ya Mji Njombe Ester Mwageni ameyataka Mashirika binafsi kuendelea kupambana na Maambukizi kuanzia ngazi za shule ya msingi ambapo wanafunzi wengi wamekuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na maambukizi huku akiisihi jamii kuendelea kuwalea watoto katika maadili.
“Tusiendelee kuzoea janga la UKIMWI. Elimu juu ya madhara ya VVU bado inahitajika kwa jamii kwa kiasi kikubwa. Wanafunzi wa Shule za Msingi wengi hawana elimu ya kutosha na wapo kwenye hatari kubwa” Alisema Mgeni
Mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Mji Njombe Daniel Mwasongwe amesema kuwa Dira ya Mapambano hayo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 ni kuwa na jamii isiyokuwa na maambukizi mapya ya VVU na kufikia 03 ambazo ni Maambukizi mapya kuwa 0,vifo vitokanavyo na VVU 0,unyanyapaa na ubaguzi wa WAVIU kuwa 0.
Kwa upande wao wawakilishi wa Mashirika yanayoshiriki katika mapambano hayo akiwemo Shedrack Mahenge Mratibu kutoka Shirika la SECO na Bariki Mhagama Mwezeshaji kutoka Shirika la COCODA wanasema kuwa licha ya kuwa jitihada zimekuwa zikifanyika kutoa elimu na kuwafikia wanufaika kwa njia mbalimbali bado changamoto kubwa imeendelea kuwa jamii hususani vijana kutokuwa na mwamko wa kutosha kushiriki katika semina na makongamano yanayohusu UKIMWI.
Aidha wameelezea kuwa kwa upande wa wadau wa mapambano hayo yapo Mashirika ambayo yamekuwa yakitoa taarifa ambazo sio sahihi kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa Wafadhili ambapo imepelekea Wanufaika wengine kuandikishwa zaidi ya mara moja na kukosekana kwa taarifa sahihi za Mnufaika katika majalada pindi Mradi unapokuwa umeisha.
Maoni yaliyotolewa na Wadau hao ni pamoja na kuhakikisha kuwa Elimu inaendelea kutolewa kwa Wanafunzi na kuhakikisha kuwa katika vikao vya maendeleo ya Shule vya wazazi agenda ya VVU inajadiliwa ili wazazi nao waweze kufahamu jukumu walilonalo kwa watoto wao.
Kikao hicho kilihusisha wadau kutoka katika Mashirika ya COCODA, HHU, DREAM, AGAPE, SECO na NSHIDA ambao wote wapo katika mapambano hayo katika Halmashauri ya Mji Njombe
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe