Naibu Waziri wa Nyumba Maendeleo ya Makazi Mhe,Angelina Mabula amewataka Watumishi wote wa Idara ya Ardhi Mkoa wa Njombe kufanya kazi kwa uzalendo na kwa kasi kutokana na kasi ndogo ya umilikishaji na upimaji jambo linalopelekea Mkoa kutokufanya vizuri. Hayo yalisemwa katika ziara yake katika Mkoa wa Njombe ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na Watumishi.
“Kasi ya kuwawezesha Wananchi kwenye sekta ya ardhi bado ni ndogo.Wizara ya ardhi ni Wizara wezeshi katika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.Kulingana na taarifa ya Mkoa kuna maeneo Halmashauri hazijafanya kazi yoyote alama za utekelezaji ni sifuri.Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani Watumishi mmejisahau katika kuwahudumia Wananchi.Hii inasikitisha kwa stahili hii hatuwezi kufika”Alisema Naibu Waziri.
Aliendelea kusema kuwa Licha ya kuwa Idara ya Ardhi inasimamia Idara za ardhi kwenye Halmashauri katika ajira na nidhamu, hiyo haibadilishi Majukumu ya Wakurugenzi kuendelea kusimamia utekelezaji na utendaji kwa Watumishi hao kwani Halmashauri ndio Mamlaka za upangaji Miji.
Aidha alielezea kuwa kumekuwa na wadaiwa sugu wa kodi za ardhi lakini kumekuwa na ufuatiliaji usioridhisha kwa kutumia sheria za ardhi jambo linaloipotezea Serikali mapato na kuwafanya wadaiwa hao kufurahia huduma za ardhi bila kulipiwa jambo ambalo ni kinyume na sheria na kuwataka watendaji kuchukua sheria zinazotakiwa ili kutokomeza tabia hiyo.
Kuhusu uhaba wa watumishi katika Sekta ya Ardhi Mheshimiwa Mabula amesema kuwa ni vyema zikaundwa timu za Mkoa kwa kushirikiana na Wataalamu wa kila Halmashauri na kufanya kazi za upimaji badala ya kutumia wapimaji wa Halmashauri pekee jambo ambalo litapelekea ongezeko la upimaji na hivyo kupelekea wigo wa kodi kuwa mkubwa.
Naibu Waziri amewataka Maafisa Mipango Miji kuhakikisha wanatambua vijiji ambavyo vinakuwa kwa kasi na hivyo kutengenza miji midogo midogo kuwapatia elimu na kuwaelekeza namna nzuri ya upangaji ili waweze kuipanga miji hiyo badala ya kufanya ujenzi holela.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mabula alipata nafasi pia ya kukabidhi hati za viwanja kwa Wananchi katika Kata za Njombe Mjini,Mjimwema na Ramadhani Halmashauri ya Mji Njombe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe