Na: Ichikael Malisa
Kwa miaka miwili mfululizo (2024 na 2025), Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kung’ara kitaaluma baada ya wanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule za sekondari za serikali kufanikisha ufaulu wa asilimia 100 kwa kupata daraja la kwanza hadi la tatu, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 99.7 iliyorekodiwa mwaka 2021.
Akitoa tathmini ya matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2025, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Njombe, Bw. Prochesius Mguli amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mpango kazi wa pamoja kati ya shule na Halmashauri, unaolenga kuinua kiwango cha ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa.
Bw. Mguli ameongeza kuwa, mchango mkubwa umetolewa na Serikali kupitia maboresho ya miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni, mabwalo ya chakula, maabara za sayansi pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu kama maji safi na umeme. Mazingira haya bora yameongeza utulivu na umakini wa wanafunzi katika masomo yao.
"Mazingira rafiki ya kujifunzia ni msingi wa mafanikio haya. Kwa mfano, Shule ya Sekondari Njombe imefanyiwa ukarabati mkubwa wa mabweni, bwalo na jiko; Yakobi Sekondari imejengewa mabweni manne ya wasichana, na Matola Sekondari imeongezewa mabweni manne pamoja na madarasa yaliyowezesha kuongezwa kwa mikondo mitatu mwaka 2025," alisema Bw. Mguli.
Ameeleza kuwa, ili kuendeleza hamasa na ushindani chanya baina ya shule, Halmashauri huwatunuku vyeti vya pongezi, zawadi na hata safari za kutalii kwa shule na walimu wanaofanya vizuri. Mfumo huu umejikita katika kutambua mchango wa kila mhusika kuanzia waalimu hadi watumishi wa kawaida.
"Menejimenti za shule zimeweka motisha ya fedha na zawadi kwa walimu na watumishi wote kuanzia kwa waalimu hadi wapishi kwani kila mmoja ana nafasi kwenye matokeo. Mwaka jana, shule ya Sekondari Uwemba na Njombe zilipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro kama sehemu ya kutambua juhudi zao," aliongeza.
Ushirikiano mzuri kati ya walimu, wazazi, wanafunzi na viongozi wa serikali umeendelea kuwa sehemu muhimu ya mafanikio haya ya kitaaluma. Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Mji Njombe imepokea zaidi ya shilingi bilioni 1.4, fedha zilizotumika kujenga shule mpya, madarasa, matundu ya vyoo, mabweni na kuboresha miundombinu ya shule za sekondari.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe