Wakulima wa mtaa wa Mpobota - Mjimwema Halmashauri ya mji Njombe wamesisitizwa kutumia mbolea kwa usahihi na kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Wito huo umetolewa Oktoba 10, 2025 na Joshua Ng’ondya kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea nchini, wakati wa kampeni maalum ya kuhamasisha wakulima kuhusu matumizi bora ya mbolea katika wilaya zote za Mkoa wa Njombe ambapo alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwajengea wakulima uelewa sahihi kuhusu namna bora ya kutumia mbolea, pamoja na kuwahamasisha kujisajili kwenye daftari la wakulima katika maeneo yao ili kunufaika na ruzuku ya mbolea inayotolewa na Serikali.
“Tunataka kupata uzoefu kutoka kwa wakulima wa Njombe kwa kuwa wengi wenu hamlimi bila kutumia mbolea. Ni muhimu mjue aina ya mbolea mnazotumia na muwe na taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wake,” alisema Ng’ondya.
Aidha, wakulima ambao hawajasajiliwa katika mfumo wa ruzuku wameshauriwa kujipatia namba maalum ya usajili kupitia Maafisa Kilimo wa maeneo yao ili waweze kunufaika na mpango wa ruzuku pamoja na kuwakumbusha wakulima kutunza risiti baada ya kununua mbolea kama uthibitisho wa manunuzi halali, ili kuepuka kuuziwa mbolea kwa bei kubwa na zisizo na ubora unaotakiwa.
Uwepo wa ruzuku hiyo unalenga kusaidia wakulima katika kukuza uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla, kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani, na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha Nchini
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe