Njombe, 14 Februari 2025 – Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa yote 463 ya mkoa huo kuhakikisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao inalindwa na kusimamiwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Mtaka alisema kuwa kuna baadhi ya miradi imekuwa ikiharibika kwa sababu ya uzembe wa viongozi wa vijiji na mitaa, jambo linalosababisha wananchi kukosa huduma bora. Alisisitiza kuwa kila mwenyekiti ana jukumu la kusimamia rasilimali zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo na kuhakikisha zinatumika kama ilivyokusudiwa.
"Kama mwenyekiti, usiruhusu mradi wowote wa maendeleo kuharibika ikiwa umepangwa kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wako," alisema Mhe. Mtaka. Aliwataka Wenyeviti wa Vijiji kushirikiana na wananchi katika kulinda na kudhibiti matumizi ya miradi ya serikali na wahisani ili kuhakikisha inaleta tija kwa jamii. Mkutano huo ulihudhuriwa na Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe, ambapo walijadili changamoto na njia bora za kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe