Wananchi wa Mtaa wa Mpobota, Kata ya Mjimwema,Halmashauri ya Mji Njombe wametakiwa kutumia haki yao ya kikatiba ifikapo Oktoba 29,2025 kwa kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi Mkuu wa kumchagua Rais,mbunge na diwani.
Akizungumza Oktoba 10,2025 na wananchi wa mtaa huo, Afisa Tarafa wa Njombe Mjini, Bi. Lilian Nyemele, aliwahimiza wananchi wote kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu ili kuchagua viongozi wanaowataka ambao watawatumikia kwa uaminifu na uadilifu. Alisema kuwa kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kila raia, kwa kuwa ni njia muhimu ya kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia viongozi wanaochaguliwa kwa demokrasia.
Aliwakumbusha wananchi wote kuendelea kuhudhuria mikutano ya kampeni za wagombea wa nafasi mbalimbali, ili waweze kusikiliza sera, mipango na vipaumbele vyao kabla ya kufanya maamuzi wakati wa kupiga kura.
Alisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa hiyo kwa umakini na kutofanya maamuzi kwa misingi ya ushabiki au upendeleo, bali kwa kuzingatia uwezo na uwajibikaji wa mgombea.
Aidha, aliwakumbusha wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu katika kipindi chote cha kampeni, siku ya kupiga kura na hata baada ya matokeo kutangazwa. Alisema kuwa tarafa ya Njombe Mjini imekuwa mfano wa amani kwa muda mrefu, hivyo hatarajii kusikia changamoto yoyote inayohusiana na uvunjifu wa amani au usalama.
“Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa uchaguzi huu unafanyika kwa amani na utulivu. Tukiepuka maneno ya uchochezi na chuki, tutakuwa tumetoa mchango mkubwa katika kudumisha umoja na mshikamano katika jamii yetu,” alisema Nyemele.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walieleza kuwa wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, huku wakiahidi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha kuwa zoezi la uchaguzi linafanyika katika mazingira salama na tulivu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe