Oktoba 8, 2025 ,Wananchi wa vijiji vya Ngalanga na Uliwa, vilivyopo Kata ya Iwungilo, Halmashauri ya Mji wa Njombe, wamepatiwa elimu juu ya ufugaji bora wa nyuki pamoja na mbinu sahihi za uvunaji wa mazao ya nyuki kama vile asali na maziwa ya nyuki.
Elimu hiyo imetolewa na Afisa Nyuki kutoka Idara ya Maliasili na Misitu, Bi. Mary Urasa, ambaye amewahamasisha wananchi kuangalia fursa zilizopo katika sekta ya ufugaji nyuki kama njia mbadala ya kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Akizungumza na wananchi hao, Bi. Urasa alieleza kuwa ufugaji wa nyuki una faida nyingi zinazochangia moja kwa moja katika uchumi wa familia na afya ya jamii kwa ujumla.
“Faida za ufugaji nyuki ni nyingi. Mbali na kupata asali na maziwa ya nyuki, wakulima wanaweza pia kunufaika na bidhaa nyingine zinazotokana na asali kama vile mafuta ya kupaka na dawa mbalimbali. Vitu hivi vina thamani kubwa sokoni na vina manufaa makubwa kiafya,” alisema Bi.Mary.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kurina (kuvuna) asali kwa wakati sahihi kutumia mbinu salama zisizodhuru nyuki wala kuharibu mizinga. Alitoa wito kwa wakulima kutumia mizinga ya kisasa ambayo ni rafiki kwa mazingira na rahisi kuvuna asali bila uharibifu.
Halmashauri ya Mji Njombe kupitia idara na vitengo mbalimbali,itaendelea kusogeza huduma za ugani karibu na wananchi, ikiwemo elimu ya kilimo, ufugaji na uhifadhi wa mazingira, ili kuwawezesha wananchi kutumia rasilimali asilia kwa njia endelevu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe