Watendaji watakaosimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma wameanza mafunzo maalum Julai 15, 2025. Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo na uelewa wa kina kuhusu majukumu yao, sheria, taratibu, miongozo ya uchaguzi pamoja na mbinu bora za usimamizi na utekelezaji wa shughuli za uchaguzi kwa kuzingatia misingi ya uhuru, haki na uwazi.
Mafunzo hayo yametanguliwa na zoezi la kula kiapo cha uadilifu, kutunza siri na kujitoa rasmi kwenye uanachama wa chama chochote cha siasa. Kiapo hicho kilitolewa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Liad Chamshama, na kilihusisha wasimamizi wa Uchaguzi wa Mikoa, wasimamizi wasaidizi ngazi ya Jimbo, pamoja na maafisa wengine watakaoshiriki katika kusimamia Uchaguzi.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 umebeba kaulimbiu isemayo: “Kura Yako Haki Yako – Jitokeze Kupiga Kura”, ikiwa ni wito kwa wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia kwa kutumia haki yao ya kikatiba.
Mafunzo haya ya siku tatu yanayoendeshwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) yanatarajiwa kukamilika Julai 17, 2025. Baada ya mafunzo haya, wasimamizi wa uchaguzi wa mikoa pamoja na wasaidizi wao ngazi ya jimbo wataendelea na utekelezaji wa majukumu yao kama ilivyokusudiwa.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe