Waalimu wa Shule za Sekondari Halmashauri ya Mji Njombe wameshauriwa kuepuka kupata ushauri wa kutumia dawa mtaani badala yake watumie bima ya afya kwenda kwenye vituo vya afya kuchunguzwa Afya zao ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Rai hiyo imetolewa na mkaguzi wa dawa kutoka Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya nyanda za juu kusini Bi Grace Kapande wakati akitoa elimu ya matumizi sahihi ya dawa na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya dawa kwa waalimu wa Shule za Sekondari Mabatini,Mbeyela ,Yakobi na Uwemba.
“Ninyi wote ni watumishi wa serikali na mna bima za afya niwaombe tumieni hizo bima kuchunguza afya zenu ,nenda hospitali usikubali ununue dawa bila kupima ugonjwa wakati bima ya afya unayo ,na uzuri sasa hivi kwenye hospitali zetu vipimo vingi vinafanyika tupime afya wapendwa”Alisema Bi Grace Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA.
Aidha Bi Grace amesema matumizi mabaya ya dawa ikiwemo kutokumaliza dozi na kutumia dawa bila kupima afya yamesababisha baadhi ya dawa kuonekana hazifanyi kazi kwasababu tayari zimetengeneza usugu wa vimelea vya magonjwa na nyingine kuharibu kabisa viungo kwenye mwili wa binadamu.
“Unapopewa dozi ya dawa na mtaalamu hakikisha unamaliza ,kumekuwa na tabia mtu anapewa dawa akinywa dozi mbili anapata nafuu anaacha,hiyo ni mbaya ndiyo inasababisha vimelea vinakuwa sugu na ugonjwa kujirudiarudia,kama dozi ni kutwa mara 3 kwa siku tano hakikisha unatumia kila baada ya saa nane bila kupunguza wala kuongeza muda hayo ndiyo matumizi sahihi dawa”Alisisitiza Bi Grace.
Kwa upande wake mwalimu wa Shule ya Sekondari Mbeyela Pulkeria Mlwale alitoa shukrani kwa TMDA kufanya mafunzo hayo nakutoa ombi kwa wafamasia wanatoa huduma kwenye vituo vya afya kuendelea kutoa elimu nakusisitiza wagonjwa kutumia dozi kwa usahihi ili kuepuka ugonjwa kujirudia na kuwa sugu.
“Elimu iliyotolewa imenigusa sana hasa kwenye muda sahihi wa kumaliza dozi ,niombe hawa wataalamu wa dawa wakati wakumpatia mgonjwa dawa watoe elimu na msisitizo ili tutumie dawa kwa usahihi kama mlivyoeleza madhara na makubwa”Alisema Mwalimu Pulkeria
Katika hatua nyingine Bi Grace Kapande mkaguzi wa dawa kutoka TMDA ametoa rai kwa waalimu kwenye shule za sekondari zilizopo Halmashauri ya Mji Njombe kuendelea kutoa elimu waliyopatiwa kwa wanafunzi na jamii ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi mabaya dawa.
Elimu ya matumizi sahihi ya dawa imetolewa na TMDA kwa waalimu na wanafunzi katika shule za sekondari Mpechi ,Mabatini,Mbeyela,Yakobi na Uwemba kuanzia Oktoba 18 ,2023 hadi Oktoba 20,2023.
Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) ni taasisi ya serikali iliyopo chini ya wizara ya afya ,maendeleo ya jamii ,jinsia wazee na watoto yenye jukumu la kudhibiti ubora ,usalama,na ufanisi wa dawa ,vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe