Novemba 6, 2025,Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Anthony Mtaka, ameongoza maombi maalum ya kuombea amani ya Taifa na Mkoa wa Njombe katika tukio lililofanyika eneo la stendi ya zamani katika Halmashauri ya Mji wa Makambako.
Maombi hayo yalihudhuriwa na wananchi kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na wadau wa maendeleo. Tukio hilo lilitanguliwa na majadiliano yaliyoongozwa na Mhe. Mtaka kuhusu madhara yanayosababishwa na vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Wananchi walipata nafasi ya kuelezea hisia zao kufuatia vurugu zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara kipindi cha uchaguzi mkuu wa 2025 na baada yake, ambavyo vilisababisha uharibifu wa mali na athari kwa watu.
Baadhi ya wafanyabiashara, akiwemo Bilnas Mtega, walizungumzia changamoto wanazokumbana nazo wakati shughuli za biashara zinasimama kutokana na vurugu, huku wakitoa pongezi kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe kwa kuchukua hatua za mapema kukabiliana na viashiria vya uvunjifu wa amani.
“Sisi machinga tunapambana kila siku ili familia ipate chakula, lakini unapokaa siku nne au tano bila kufanya kazi inaathiri sana maisha yetu,” alisema Mtega.
Naye Jestina Singaile aliwataka wanawake kuendelea kuombea Taifa na viongozi, akisisitiza umuhimu wa kudumisha maombi na upendo ili kuzuia vurugu na chuki katika jamii.
"Wanawake tuache kushabikia haya mambo ,hatuwezi sisi,tudumu katika maombi ,tukikaa magotini Mungu atatupa majibu sahihi ,tutafute amani na uzima ,tupendane tusinyoosheane vidole,tudumu katika maombi nchi itakuwa salama"Alisema.
Baada ya mjadala na maombi, Mhe. Mtaka aliwataka wananchi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Njombe kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa utulivu, akisisitiza kuwa matukio ya misukosuko yaliyotokea katika mikoa mingine yamepita na hayapaswi kuleta hofu.
Alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi wote kuendeleza mshikamano, upendo, na maombi kwa ajili ya kulijenga Taifa lenye amani na utulivu wa kudumu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe