Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Njombe Mjini Bw.Samson Medda Oktoba 26,2025 amefungua rasmi mafunzo kwa watendaji 1,046 ambao wameteuliwa kuwa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura yatakayodumu kwa siku mbili kuanzia Oktoba 26 hadi 27, 2025.
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watendaji kuhusu wajibu na majukumu yao vituoni, taratibu za upigaji kura, pamoja na mambo muhimu ya kuzingatiwa kabla, wakati, na baada ya kupiga kura. Vilevile, washiriki wanapewa mafunzo juu ya taratibu za kuhesabu kura na matumizi sahihi ya vifaa vya uchaguzi.
Katika ufunguzi wa mafunzo hayo, watendaji wote walikula kiapo cha uadilifu na kuapa kujitoa uanachama wa chama chochote cha siasa, kama sehemu ya kuhakikisha usimamizi huru na wa haki wa uchaguzi.
Mafunzo hayo yanakuja ikiwa zimesalia siku tatu pekee kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Msimamizi wa Uchaguzi amewataka washiriki kuyachukua mafunzo hayo kwa umakini na uzalendo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, uwazi, na ufanisi, kwa kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi.
Bw. Medda alisisitiza "Someni kwa makini katiba,sheria,kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa ,jiepusheni kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka vyama vya siasa ,fanyeni kazi kwa ushirikiano kama team ,hakikisheni mna hakiki vifaa na kuvitunza,hakikisheni mnafika kwa wakati kwenye vituo mlivyopangiwa"
"KURA YAKO HAKI YAKO JITOKEZE KIPIGA KURA"
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe