Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bi.Christina Mndeme, amezitaka taasisi zote za Mkoa wa Njombe kuhakikisha zinatumia nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira dhidi ya ukataji miti kiholela.
Mndeme ametoa wito huo Tarehe 21 Agosti, 2024, katika mkutano wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia uliowahusisha viongozi wa taasisi mbalimbali Mkoani Njombe.
Katika hotuba yake,aliitaka jamii kuhakikisha inatumia nishati safi ili kulinda mazingira kutokana na ukataji miti holela unaosababishwa na matumizi ya nishati zisizo salama.
Aliongeza kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ruzuku ya nishati safi, itakayosaidia Watanzania wenye hali duni kupata nishati hiyo kwa urahisi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kulinda mazingira.
Aidha alifafanua kuwa moshi unaotokana na matumizi ya nishati zisizo safi huwa na gesi zenye sumu pamoja na chembechembe ndogo za vumbi zenye viambato hatari ambavyo vinaweza kudhoofisha mfumo wa upumuaji na kusababisha magonjwa sugu kama kikohozi, homa ya mapafu, kifua kikuu, pumu, na saratani ya mapafu.
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni njia bora ya kulinda afya ya jamii na mazingira kwa ujumla, hivyo taasisi zote zinapaswa kuchukua hatua stahiki kwa kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha malengo ya kutumia nishati safi yanatimia.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe