Shule ya msingi Nazareth iliyopo kata ya Mji Mwema Halmashauri ya Mji Njombe imefikia lengo la kuandikisha wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza kwa asilimia 100 mwaka 2024.
Akitoa taarifa ya shule hiyo Januari 17,2024 kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe.Anthony Mtaka aliyefanya ziara shuleni hapo ,Mkuu wa shule ya Msingi Nazareth Mwalimu Onani Luponelo Myenda amesema malengo ya uandikishaji shuleni hapo yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi 84 wa darasa la awali na wanafunzi 109 wa darasa la kwanza na kwamba hadi sasa wamevuka lengo kwa kuandikisha na kupokea wanafunzi 86 wa darasa la awali na wanafunzi 128 wa darasa la kwanza.
Akizungumzia kuhusu taaluma shuleni hapo Mwalimu Myenda amesema, kiwango cha ufaulu kwa darasa la nne na darasa la saba kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2020 ni zaidi ya asilimia 90.
Aidha ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule hiyo fedha kiasi cha shilingi milioni 56 kwa kipidi cha mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu matatu ya vyoo kupitia mradi wa BOOST.
Akitoa takwimu za jumla za uandikishaji wa darasa la awali na darasa la kwanza kwa halmashauri ya Mji Njombe Afisa Elimu Halmashauri ya Mji Njombe Bi.Shida Kiaramba amesema mpaka sasa darasa la awali wamepokelewa wanafunzi 3316 sawa na asilimia 71 yakundikisha wanafunzi 4639 na darasa la kwanza wamepokelewa wanafunzi 3924 sawa na asilimia 89 ya kuandikisha wanafunzi 4408.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi Kuruthum Sadick amewahakikishia waalimu na wanafunzi wa kuwa changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo shuleni hapo imefanyiwa kazi na mwaka wa fedha ujao 2024/2025 yataongezwa matundu 20 ili yatosheleze kuhudumia wanafunzi wote shuleni hapo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka, amepongeza uongozi wa shule ya Msingi Nazareth na Halmashauri kwa namna ambavyo suala la taalama linasimamiwa vizuri shuleni hapo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe