Akizungumza wakati wa mafunzo yaliyolenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto katika Halmashauri ya Mji Njombe, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Ruth Msafiri ameitaka jamii kutambua kuwa swala la ulinzi na usalama wa mtoto ni jukumu la jamii nzima hivyo ni vyema jamii kuzifahamu na kuzijua haki za mtoto na kuhakikisha kuwa inazilinda.
“Kumekuwa na matukio mengi ya ukatili kwa watoto kwa siku za karibuni yakiwemo ya kingono, kimwili, kutelekezwa, unyonyaji, usafirishaji haramu wa watoto, ukeketaji na ndoa za utotoni. Matukio haya yanasikitisha sana, ni vyema tukaona namna ya kuanzisha balozi wa mtoto ambaye atakua rafiki wa watoto na ambaye atakuwa mwaminifu na mwadilifu, awe tayari kuonya na kukemea maovu yote yanayofanyika kwa watoto ambaye mtoto anapopatwa na tatizo aweze kumwelezea na afahamike katika jamii husika” Alisema Mkuu wa Wilaya.
Kwa mujibu wa sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 kifungu kidogo cha 5, inazipa mamlaka za serikali za mitaa mamlaka ya kulea, kulinda na kutunza watoto walioko katika Halmashauri zao. Hivyo ni wajibu wa madiwani wakiwa na mwenyeviti wao kama viongozi wa siasa kuhakikisha wanawalea watoto kutoka katika ngazi ya Kata hadi Halmashauri.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Njombe George Emmanuel amesema kuwa ni vyema sheria inayolenga kutoa adhabu kwa serikali za mitaa kutotekeleza wajibu kulipa faini isiyozidi elfu hamsini, kifungo cha miezi mitatu au yote kwa pamoja kuangalia vyema na kufanya mabadiliko ya sheria hii kulingana na Mazingira ya sasa kwani adhabu hii ni ndogo ukilinganisha na matatizo yanayoweza kujitokeza pale ambapo Halmashauri inashindwa kutekeleza jukumu la kuwalinda watoto walioko kwenye Halmashauri zao.
Kikao hicho pia kimeazimia kuhakikisha kuwa Halmashauri inatenga fedha katika bajeti ijayo kuanzisha mchakato wa ujenzi wa kituo cha watoto kijulikanacho kama one stock Centre ambapo huduma za kisheria,kimalezi na huduma zote zinazomuhusu mtoto zitakuwa zinapatikana katika kituo hicho.
Hosea Yusto ni Afisa Ustawi Halmashauri ya Mji Njombe amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2017/2018 kesi 54 za ukatili dhidi ya watoto zilifikishwa mahakamani kwa upande wa Halmashauri ya Mji Njombe na Halmashauri imeanzisha mpango wa kutoa mafunzo kwa Wahe. Madiwani kuhusu kuzuia ukatili wa watoto lakini pia Halmashauri imepanga kuanzisha na kutoa mafunzo kwa timu za ulinzi wa mtoto na kuwapatia watoto mafunzo yatakayoweza kuwajengea uwezo wa kujilinda na kuwalinda wenzao.
Aidha, kupitia mafunzo hayo Halmashauri imelenga kuanzisha progamu ijulikanayo kama “Balozi wa Mtoto” itakayowezesha kupatikana kwa balozi kuanzia kila ngazi ikianzia familia mpaka kwenye Halmashauri ili kuweza kupata mabalozi watakaokuwa wasemaji wa watoto na kukemea ukatili dhidi ya watoto. Mafunzo hayo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji njombe yaliwahusisha Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri pamoja na wadau mbalimbali.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe