Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili Majibu na Utekelezaji wa Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali za mwaka 2022/2023 unaendelea katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Akiwasilisha majibu na utekelezaji wa hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi.Kuruthum Sadick amesema Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kudumu kwa kupata hati safi kwenye Hesabu kuu za Halmashauri,Hesabu za mradi wa mfuko wa Afya wa pamoja (Health Sector Busket Fund) na Hesabu za Mfuko wa Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu (WYDF) ,kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 – 2022/2023.
Ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hoja 15 kati ya 30 zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zimejibiwa, kuhakikiwa na kufungwa na hoja zilizobaki zipo kwenye utekelezaji zikisubiri uhakiki wa Mkaguzi kwa awamu ya pili.
Kwa upande wa hoja zinazohusu mfuko wa wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu amesema hoja 5 zimefungwa na hoja 3 zipo kwenye utekelezaji zikisubiri uhakiki wa Mkaguzi wa awamu ya pili na utekelezaji wa maagizo 2 ya kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) unaendelea.
Aidha amesema mikakati ya Halmashauri kufunga hoja zilizobaki ni pamoja na kuchukua hatua za sheria na ufuatiliaji kwa wadaiwa wote ambao hawajalipwa madeni ili madeni hayo yalipwe, kuwajengea uwezo watumishi katika maeneo yao ya kazi kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yanayohusu utendaji kazi ili kupunguza uibukaji wa hoja na kuhakikisha hoja zote zinafungwa kufikia mwezi, Septemba 2024.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe