Serikali kupitia mradi wa TACTICS awamu ya pili inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 20.7 kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami awamu ya kwanza katika Halmashauri ya Mji Njombe. Mkandarasi anayesimamia utekelezaji wa mradi huo China National Aero Technology International Engineering Corporation, amekabidhiwa rasmi maeneo ya ujenzi (saiti) Julai 23,2025 tayari kuanza kazi.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilomita 8.4 zitakazojengwa kwa kiwango cha lami sambamba na uwekaji
wa miundombinu ya kisasa ikiwemo ujenzi wa ofisi ya mradi yenye gorofa moja,madaraja na taa za barabarani. Mkataba wa ujenzi una muda wa miezi 15, hivyo barabara zinatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026.
Miongoni mwa barabara zitakazojengwa ni barabara ya NBC-Kibena km 2.84,Chaugingi - Nzengerendete - km 1.57,Nzengerendete-Masaki km 1.43
,Magereza-Matalawe km 1.12 na barabara ya Mpechi-Melinze KM 1.3
Baadhi ya wananchi waliokusanyika kushuhudia makabidhiano hayo katika maeneo mbalimbali ya mradi, wameishukuru Serikali kwa kuwaletea maendeleo na kuomba mkandarasi kuzingatia muda uliopangwa ili
kukamilisha mradi kwa wakati.
Kwa upande wake, Mhandisi Costastine Bengwe kutoka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Njombe, ambaye ni msimamizi wa mradi huo, amesisitiza mkandarasi kuzingatia masharti ya mkataba na kufanya kazi kwa viwango vinavyostahili. Ameeleza kuwa TARURA iko tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora na kwa wakati.
Mbali na maboresho ya miundombinu, mradi huo unatarajiwa kuleta fursa mbalimbali kwa wakazi wa Mji wa Njombe, ikiwemo ajira rasmi na zisizo rasmi kwa kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.
“Tunategemea kuona si tu barabara bora, bali pia kuona wananchi wa hapa wakinufaika kiuchumi kupitia ajira zitakazopatikana,” amesema Mhandisi Costastine.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya barabara, kuinua uchumi wa wananchi na kuboresha taswira ya miji kwa maendeleo endelevu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe