Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema kuwa Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 7.65 kwa ajili ya kuanza rasmi hatua ya pili ya ujenzi wa majengo kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Hayo yamesemwa na Waziri Ummy wakati wa uzinduzi wa huduma katika Hospital mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ambapo amezindua rasmi shughuli za utoaji huduma katika Hospitali hiyo. Uzinduzi huo uliambatana na kukabidhi iliyokuwa Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa Kibena kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka ambaye naye aliikabidhi kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji Njombe kwa ajili ya kuendelea na utaratibu wa kuiendesha Hospitali hiyo kama ilivyokuwa awali.
“Rais Magufuli ametupatia shilingi bilioni 7.65 kwa ajili ya hatua ya pili ya ujenzi wa hospitali hii mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe hatua ambayo itahusisha ujenzi wa majengo mengine saba. Leo hapa ninamkabidhi eneo la ujenziwa majengo hayo Mkandarasi aanze kazi mara moja na ndani ya miezi 8 mpaka 10 awe amekamilisha ujenzi wa majengo hayo kwani fedha ipo ya kutosha. Serikali imepanga kuleta madaktari bingwa wa fani 13 pamoja na vifaa vya kisasa kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.” Alisema Waziri Ummy.
Katika kuendelea kuboresha huduma za Afya Mkoani Njombe Waziri Ummy ameuhakikishia uongozi wa Halmashauri ya Mji Njombe kuwa Hospitali ya Kibena itaendelea kutumia bajeti ya awali iliyokuwa inatumiwa ikiwa kama Hospitali Teule ya Rufaa ambayo ilikua ni kiasi cha Shilingi milioni 280 na amesema kuwa hakuna kifaa tiba chochote kitakachoondolewa katika Hospitali ya Kibena kupelekwa katika Hospitali mpya ya rufaa.
“Napenda kuipongeza Halmashauri kwani hamkufanya makosa kukabidhi Hospitali ile ya Kibena itumike kama Hospitali ya Rufaa. Ninyi wenyewe ni mashahidi baada ya kuwa imeteuliwa kuwa Hospitali Teule ya Mkoa hali ya utoaji huduma ilibadilika kwa kiasi kikubwa. Ni matumaini yangu kuwa Halmashauri mtaendelea kuboresha utoaji huduma katika Hospitali ya Kibena ili ipatikane huduma bora zaidi na sisi tutaendelea kushirikiana na ninyi ili kuendelea kuihudumia” Waziri Ummy
Wakizungumza kwa wakati tofauti tofauti, baadhi ya Wananchi waliohudhuria katika uzinduzi wa huduma wameipongeza Wizara ya Afya na Serikali ya awamu ya tano kwa hatua wanazoendelea kuchukua za kuhakikisha kuwa huduma ya afya zinaboreka na kuimarika katika Mkoa wa Njombe kwani Mkoa wa Njombe, ni miongoni mwa Mikoa iliyokuwa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa lakini sasa hali inaendelea kuboreka kila siku.
Ujenzi wa jengo la wagonjwa wa huduma za nje ambalo huduma katika jengo hilo imezinduliwa na Waziri Ummy imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 3.2 mpaka kukamilika kwake.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe