Na Ichikael Malisa
Vijana 600 kutoa wilaya ya Njombe Aprili 05,2024 wametambulishwa fursa mbalimbali kwenye sekta ya kilimo, biashara, ujasiriamali na ufugaji zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi badala yakutegemea ajira.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la fursa kwa vijana lililoambatana na utambulisho wa programu ya kuwawezesha vijana,Mkuu wa Wilaya ya Njombe,Mhe. Kissa Gwakisa amesema kongamano hilo ni maalumu kwa vijana kuzitambua fursa zilizopo kwenye kilimo haswa kilimo cha mazao ya muda mfupi na namna wanavyoweza kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo cha mazao hayo.
Ametoa wito kwa vijana kuzipokea fursa hizo na kwa wote watakaowezeshwa kwenye fursa mbalimbali kuwa na nidhamu itakayowezesha kutimiza lengo la programu hiyo la kuhakikisha vijana wanafanya kazi na kujikwamua kiuchumi.
Mhe.Kissa ameeleza kuwa programu yakuwawezesha vijana ni endelevu na inaanza kwa kutoa tani 28 za mbegu za ngano kwa vijana sambamba nakuwawezesha vijana wengine 600 kwenye shughuli mbalimbali.
Aidha amewataka vijana kuwa makini na utapeli mitandaoni unaotangaza fursa za kitapeli kwa kutumia majina ya viongozi, badala yake watumie ofisi na wataalamu waliopo kwenye maeneo yao kwa taarifa mbalimbali zinazohusu fursa.
Akizungumza kwa njia simu,Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, vijana,ajira na wenye ulemavu Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa pongezi kwa ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Njombe kwa kuona umuhimu wa kutambulisha na kuwawezesha vijana kwenya fursa mbalimbali.
Aidha amesema Serikali imetengeneza fursa za kutosha kwa vijana kwenye sekta mbalimbali akiwataka vijana kuchukua hatua kuzichangamkia ili kujikwamua kiuchumi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe