Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mheshimiwa Kissa Gwakisa ameipongeza Halmashauri ya Mji Njombe kwa kuwa kinara wa makusanyo kwenye Halmashauri za miji ambapo ameahidi kutoa ushirikiano na kuhakikisha Halmashauri Inaendelea kushikilia nafasi hiyo.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Salamu za Serikali katika Mkutano wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani kwa robo ya nne Kissa amesema kuwa Baraza la Madiwani,na Wataalamu wameomesha Ubunifu na Uzalendo wao katika kuhakikisha kuwa Halmashauri inafanya vizuri kwenye makusanyo.
"Ripoti ya Mheshimiwa Waziri kuhusu Makusanyo imedhihirisha wazi kuwa mnafanya Kazi. Napenda niwapongeze sana na niwaombe mkasimamie nafasi ambayo mmeipata. Zipo Halmashauri nyingine nazo zitakuja kwenye ushindani muhakikishe kuwa mnaishikilia nafasi hiyo.
Awali akitoa hotuba ya ufunguzi katika Baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri Erasto Mpete amesema kuwa Halmashauri imefanikiwa kuwa na zidio la makusanyo ya Shilingi Bilioni 1.5 na hii ikiwa ni kutokana na kuweza kuvuka Lengo la Makusanyo.
Katika hatua nyingine wakati wa kujadili taarifa za Kamati mbalimbali miongoni mwa hoja zilizojadiliwa kwa kina ni uanzishwaji wa Shule ya Msingi yenye mchepuo wa Kiingereza ambapo licha ya Kamati ya Uchumi Afya na Elimu kutoipa kipaumbele baadhi ya Madiwani wamesema hiyo ni kukatisha tamaa Wataalamu ambao wamekuwa wakihangaika kuandaa maandiko
“Wazo lilikuwa jema, Wataalamu wamekuwa wabunifu kuleta andiko hilo. Mimi ningeshauri kuwa wazo hilo kwa sasa lingesubiri kutokana na kwamba Halmashauri kwa sasa inamiradi mingi ya ujenzi na bado kuna Shule nyingi za Msingi zinahitaji kujengwa upya kutokana na miundombinu yake kuwa chakavu. Shule hii itahitaji Waalimu. tunachangamoto kubwa ya Waalimu. Hata Mimi katika Kata yangu hawajitoshelezi na tukianzisha Shule mpya itatubidi Waalimu hao tulionao kuwagawa jambo ambapo tutakuwa tunawapa mzigo Waalimu. Mimi naona wazo ni jema ila lisubiri tukamilishe miradi hii mikubwa ambayo zaidi ya robo tatu ya michango yake ni nguvu ya Halmashauri.” Alisema Mwanzinga Diwani wa Kata ya Matola.
Katika Mkutano huo wa Baraza baadhi ya agenda mbalimbali ziliweza kujadiliwa ambapo Moja katika ya agenda iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Thadei Luoga ilikuwa ni ile ya Baraza la Madiwani kupitisha mchakato wa Halmashauri kuwa Manispaa.
Akiwasilisha agenda hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri alisema kuwa mara baada ya kupitia vigezo mbalimbali kubwa ikiwa ni ukusanyaji mapato imeona Halmashauri inafaa kupanda hadhi na kuwa Manispaa kwani inakidhi vigezo vilivyo vingi.
Wakichangia katika hoja hiyo baadhi ya Madiwani akiwemo Diwani wa Kata ya Matola Edwin Mwanzinga na Kata ya Ramadhani Nickson Nganyange wamesema kuwa licha ya kuwa wanaunga mkono hoja bado kuna ujenzi holela ndani ya Halmashauri,ujenzi wa mabanda ya Miti,uwepo wa makontena na ujenzi usiofuata mpango kabambe wa Halmashauri jambo linaloharibu taswira ya Mji.
"Tunaelekea kuwa Manispaa makontena yote yaliyopo mjini yanatakiwa yaondolewe. Kuna vibanda vya mbao kwa ajili ya biashara mbalimbali katika eneo la Mji hivyo vyote vinatakiwa viondoke ili Mji uwe na hadhi ya Manispaa. Hatuwezi kuwa Manispaa kila sehemu kuna vibanda Alisema Mwanzinga
Diwani wa Kata ya Mjimwema Nestory Mahenge amesema kuwa bado kuna maeneo ya mjini yana uwepo wa vichaka vinavyotumika kwa ajili ya uhalifu na matukio mbalimbali na hivyo ameomba wenye maeneo yao kuhakikisha yanasafishwa na kufanya ujenzi katika maeneo hayo kwani usafi wa Mji na mazingira yanayozunguka Mji Ni vigezo muhimu kwenye Manispaa.
Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika amesema kuwa kwa kipindi kirefu kumekuwa na mvutano wa kimaamuzi kati ta Wataalamu na Wanasiasa jambo lililopeleke kucheleweshwa kwa maendeleo katika Njombe.
“Hoja za Madiwani za Halmashauri kuwa Manispaa ni hoja za Msingi. Na kwenye Kampeni Wananchi waliomba Njombe kuwa Manispaa. Na tuliwaahidi kuhakikisha kulisimamia hilo na kuliwasilisha katika ngazi mbalimbali za maamuzi. Hoja yangu pia inajikita katika kuonesha mchango wa Njombe kwenye uchumi wa Taifa” Alisema Deo Mwanyika Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini
Agenda ya Kuipandisha Halmashauri kuwa Manispaa iliungwa Mkono na Madiwani wote na sasa taratibu zinaendelea ili kuweza kufanikisha lengo Hilo
|
|
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe