Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kissa Gwakisa ameoneshwa kusikitishwa na mwamko mdogo wa Wananchi kujitokeza kuchanja katika Wilaya ya Njombe ambayo mpaka sasa Wilaya hiyo kushindwa kufanya vizuri kwenye zoezi la uchanjaji wa chanjo ya UVIKO 19 katika Mkoa wa Njombe na hivyo kufanya kikao hicho kwa lengo la kujengeana uwezo,kuhamasishana na kufanya utekelezaji wa kuhakikisha chanjo zinafikia jamii na jamii inachanja.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya CCM Wilaya, Waheshimiwa Madiwani na Wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Mji Njombe Mkuu wa Wilaya ya Njombe amesema kuwa Wilaya ya Njombe bado ipo nyuma kwenye zoezi zima la uchanjaji jambo linaloishushia hadhi Wilaya hiyo kutokana na Wilaya hiyo kuwa inaongoza katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo na amewataka Viongozi na Wataalamu kuchukua hatua za haraka kwa kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha uchanjaji.
“Tunatamani tufike mahali maisha yarudie kama yalivyokuwa awali. Tuache kuvaa barakoa, kutumia vitakasa mikono na hii yote itafanikiwa kama tutachukua hatua za kuchanja.Tushirikiane kwa pamoja na tutoe elimu sahihi kwa jamii juu ya chanjo ya UVIKO 19.”Alisema Mkuu wa Wilaya.
Awali akitoa taarifa ya hali ya uchanjaji katika Halmashauri ya Mji Njombe Mratibu Chanjo wa Halmashauri Simon Ngassa amesema kuwa malengo makuu ya chanjo ni kupambana na ugonjwa, kupunguza maambukizi ya Ugonjwa na kupunguza vifo vitokanavyo na UVIKO 19.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa changamoto kubwa zilizokuwepo katika zoezi hilo ilikuwa na uhamasishaji mdogo kwenye jamii,uwepo wa vituo vichache vya uchanjaji,ukosefu wa rasilimali na imani mbalimbali potofu kwa jamii juu ya chanjo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Njombe Edward Mgaya amesema kuwa maendeleo ya Nchi yanatokana na watu na endapo watu watakufa kutokana na ugonjwa wa CORONA ilihali chanjo ipo hakutakuwepo na maendeleo kwenye Nchi.
“Kama tupo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tunatekeleza Ilani ya Chama hatuna budi kuelimisha jamii kuchukua hatua na kuchanja.Elimu ni jambo la pekee linalohitajika kwa jamii yetu ili waweze kuchanja.Naamini wengi wanapenda kuchanja ila ukosefu wa elimu ya kutosha ndio umepelekea zoezi hili kutokufanya vizuri katika Halmashauri yetu.”Alisema Mgaya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmasahuri ya Mji Njombe Dkt. Yesaya Mwasubila amesisitiza kuwa jamii imekuwa na iamani potofu na kuwa na hofu juu ya usalama wa chanjo hiyo ambapo amesema kuwa chanjo hiyo ni salama na imethibitishwa na Shirika la Afya duniani kuwa ni salama na mpaka sasa katika Halmashauri yake hajapokea malalamiko yoyote kwa watu waliochanjwa kudhurika au kupata matatizo yoyote yaliyosababishwa na chanjo hiyo.
Wakitoa michango yao kwa nyakati tofauti tofauti Diwani wa Kata ya Mjimwema Mahenge amesema kuwa kupitia kikao hicho nae amehamasika kwenda kuchanja na amesema kuwa ukosefu wa elimu sahii ndio kikwazo kikubwa kwenye zoezi zima la uchanjaji na kuomba elimu na huduma ya chanjo kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi kupitia huduma tembezi.
Kwa upande wake Mheshimiwa Angela Mwangeni Viti Maalumu Njombe Mjini amesema kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliohamasika na kupata chanjo na hii imetokana na elimu ambayo amekuwa akiipata ya umuhimu wa chanjo.
George Emmanuel Katibu Tawala Wilaya ya Njombe amewataka viongozi wa Halmashauri ya Mji Njombe wakiwemo Waheshimiwa Madiwani kuhakikisha kuwa wanaonyesha njia kwa jamii kwani jamii imekuwa ikiwatazama viongozi hao kwa yale wanayoyafanya na kuwataka kueneza mazuri ya chanjo kwa jamii na kuihamasisha jamii kuchanja na kutoa elimu potofu zilizojengeka miongoni mwa Wananchi.
Mpaka sasa Halmashauri ya Mji Njombe inavituo 71 vya kutolea chanjo vituo 45 vikiwa vinatoa huduma ya chanjo kila siku ambapo mpaka kufikia tarehe 04/10/2021 idadi ya watu waliochanja ni 1621 ambayo ni sawa na asilimia 35.1 ya lengo ya dozi iliyotolewa ambapo mikakati iliyofikiwa katika kikao hicho ni kuendelea kutoa elimu na kusambaza chanjo kwa Kata zote 13 ili kurahisisha upatikanaji.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe