Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Sweda, ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa viashiria vya Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika Julai 24, 2025. Kikao hicho kimewakutanisha Wakurugenzi ,maafisa lishe, watendaji wa kata, na wawakilishi kutoka idara mbalimbali zinazohusika na masuala ya lishe katika Wilaya ya Njombe.
Akizungumza katika kikao hicho, DC Sweda amewataka maafisa lishe katika Wilaya ya Njombe kuongeza bidii na kuendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya udumavu, akisisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa hayapaswi kurudi nyuma.
“Ishu ya lishe ni ya nchi nzima, siyo ya Halmashauri peke yake. Mheshimiwa Rais aliweka msisitizo na sisi tukasaini mkataba wa mapambano dhidi ya udumavu kwenye maeneo yetu. Haya mambo tukiamua kuyamaliza, tunayamaliza,” alisema DC Sweda.
Aidha, amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya maafisa lishe, watendaji wa vijiji, kata, na idara zingine muhimu ili kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa afua za lishe.
“Kuna watendaji wa vijiji, mitaa na kata – tumeanza vizuri. Kila mtu asimame kwenye nafasi yake,” aliongeza.
Pia, DC Sweda amesisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu ya lishe kwa vitendo, hasa kwa wanawake wajawazito na wale wenye watoto chini ya miaka mitano. Amesema elimu hiyo inapaswa kutolewa kwa njia ya vitendo ili kuwajengea uelewa na uwezo wa kuchukua hatua stahiki katika malezi bora ya watoto na familia kwa ujumla.
Ametoa wito kwa maafisa lishe kushirikiana na madaktari na vituo vya afya kuhakikisha elimu ya lishe inatolewa kliniki kwa wajawazito, hatua itakayosaidia katika kupunguza viwango vya udumavu na kuboresha afya ya jamii.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe