Julai 04,2025,Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, amezindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo ya ruzuku kwa mifugo katika Halmashauri ya Mji Njombe. Uzinduzi huo umefanyika kwa kumchanja moja kwa moja mfugaji Joseph Kimwayeya, ambapo jumla ya ng’ombe 11 na kuku 11 wamepatiwa chanjo.
Kupitia mpango huu, Halmashauri ya Mji Njombe inatarajia kuchanja jumla ya ng’ombe 27,000 dhidi ya homa ya mapafu na kuku 200,000 dhidi ya magonjwa ya mafua makali, kideri na ndui. Chanjo kwa kuku inatolewa bure, huku kwa ng’ombe mfugaji anachangia kiasi cha shilingi 500 kwa kila dozi badala ya shilingi 1000.
Zoezi hilo linaenda sambamba na uwekaji wa hereni za kielektroniki kwa ajili ya utambuzi wa mifugo, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa mifugo na kusaidia wizara kuwa na takwimu sahihi za mifugo nchini.
Pamoja na uzinduzi huo Dkt Mhede amekabidhi vifaa vitakavyotumika kutekeleza zoezi hilo ikiwemo vishikwambi kwa ajili yakujaza taarifa za mfugaji na mifugo yake kwenye mfumo,hereni na kifaa cha kubania pamoja na chanjo kwa ajili ya ng’ombe na kuku.
Utoaji wa chanjo hizi ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupambana na vifo vya mifugo nchini. Tarehe 16 Juni 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi chanjo za magonjwa matano ya kipaumbele ikiwa ni pamoja na: homa ya mapafu, sokota ya mbuzi (PPR), ndui ya kuku (fowl pox), mafua makali ya kuku (infectious coryza), na kideri (Newcastle disease).
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe