Juni 10, 2025 ,Wananchi wa kijiji cha Mfereke walipatiwa elimu ya umiliki wa ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi za kijiji kwa lengo la kupeana taarifa za maendeleo ya kijiji pamoja na kuwajengea wananchi uelewa kuhusu masuala ya ardhi kama njia mojawapo ya kuimarisha maendeleo ya kijiji.
Katika mkutano huo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ardhi na Mipango miji H/Mji Njombe, Emmanuel Luhamba alitoa elimu kuhusu masuala ya ardhi ikiwemo umuhimu wa kupanga, kupima na kumiliki ardhi kisheria pamoja na faida zake kiuchumi na kijamii. Elimu hiyo imelenga kuwajengea uelewa wakazi wa Mfereke kuhusu matumizi bora ya ardhi na nafasi ya ardhi katika kuinua kipato chao.
"Kupanga na kupima ardhi ni hatua muhimu ya kuleta maendeleo ,inasaidia Umiliki halali wa ardhi na kumuwezesha mwananchi kupata mikopo, kuwekeza bila hofu, na kuhakikisha ardhi inatumika kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho," alisema Emmanuel Luhamba
Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wananchi wa Mfereke anayeishi nje ya kijiji alitoa wito kwa wakazi wa Mfereke kuchangamkia fursa zilizopo katika maeneo yao.
“Changamkieni fursa za kiuchumi kwenye maeneo yenu. Ipeni elimu kipaumbele kwa sababu nchi yetu bado ni miongoni mwa nchi zinazotoa elimu kwa gharama nafuu. Wapelekeni watoto shule,” alisisitiza.
Aidha, aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa katika sekta ya ardhi akieleza kuwa, “Kila muda unaopita haurudi utumieni kuzalisha mali.” Alisisitiza pia umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Kwa upande wa usalama, alitoa rai kwa wananchi kudumisha ulinzi wa kijiji chao kwa kushirikiana kwa karibu. “Kijiji cha Mfereke kinajulikana kwa ulinzi, na hili ni muhimu ili mali zetu ziwe salama.”
Katika hatua ya kuunga mkono maendeleo ya kijiji,Herbeth nziku aliahidi kujitolea kugharamia kuweka mfumo wa umeme kwnye nyumba ya mwalimu akieleza kuwa umeme tayari umepita nyumbani kwake na yeye ni miongoni mwa wanufaika wa huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji Venance Ngole alitoa shukrani kwa wananchi wazawa wa Mfereke waliopo ndani na nje ya kijiji kwa kuendelea kuonyesha moyo wa uzalendo na kukumbuka walikotoka. Alisisitiza kuwa mshikamano wa jamii hiyo utaendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio yao ya kijamii na kiuchumi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe