Kuelekea msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, Idara ya Kilimo Halmashauri ya Mji wa Njombe Oktoba 08,2025 imetoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na mbegu bora kwa wakulima katika vijiji vya Ngalanga na Uliwa, vilivyopo katika Kata ya Iwungilo.Pamoja na elimu hiyo wakulima hao walifundishwa mbinu bora za utunzaji wa ardhi kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Afisa Kilimo, Ndg.Baraka Mlawa, alieleza kuwa lengo la elimu hiyo ni kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia bora na sahihi za kilimo akitoa wito kwa wakulima wa zao la parachichi kuwa wavumilivu wakati wa kuuza mazao yao, kwani wengi huuza kwa bei ya chini sana inayowasabahishia hasara.
Wakulima hao walikumbushwa kununua mbolea kutoka kwa mawakala waliothibitishwa vijijini kwa bei elekezi, na kuwasilisha taarifa kwa viongozi wa kijiji, kata au wataalamu wa kilimo endapo watakutana na changamoto yoyote kuhusu upatikanaji au bei ya pembejeo hizo.
Wananchi walionufaika na elimu hiyo walitoa shukrani zao kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa kuhakikisha wataalamu wa kilimo wanawafikia wakulima moja kwa moja vijijini na kuwapatia elimu muhimu kuhusu kilimo bora, bei sahihi ya mbolea na mazao kama parachichi, jambo ambalo litasaidia kupata tija kwenye kilimo wanachofanya.
Walieleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia mbolea bila uelewa sahihi wa matumizi yake, hali iliyochangia uzalishaji usioridhisha. Aidha walitoa ombi kwa Serikali na wataalamu wa kilimo kuwasaidia kupima udongo ili waweze kulima kwa kuzingatia aina ya udongo na mbegu zinazofaa.
“Tunashukuru sana kwa elimu hii. Huku vijijini tumekuwa tukilima kwa mazoea bila kufuata taratibu za kilimo bora. Tunaomba Serikali itupe msaada wa kupima udongo ili tujue ni mbegu gani zinafaa, maana wakati mwingine tunapanda mazao hayazai kama tunavyotarajia, hatujui kama shida ni mbegu au mbolea,”. Alisema mmoja wa wakulima wa Kijiji cha Ngalanga.
Elimu hiyo inaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri ya Mji Njombe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe