Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka Maafisa Elimu ya Watu wazima mkoa wa Njombe kujielekeza katika mitaala mipya ya elimu ili kuendana na mabadiliko ya kidijitali na mahitaji ya sasa kwenye jamii.
Akizungumza Septemba 8, 2025, katika maadhimisho ya wiki ya Elimu ya watu wazima mkoa wa Njombe, Mhe. Mtaka amewataka maafisa elimu kuhakikisha wanaandaa mafunzo yanayoendana na mitaala ya sasa, kwa kuzingatia kasi ya kidijitali. Amesema elimu hiyo inapaswa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa ujasiriamali, matumizi ya TEHAMA na mbinu za kujiongezea kipato ili kupunguza umasikini na kukuza maendeleo ya jamii.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote waliokosa fursa ya kusoma kwa changamoto mbalimbali, ikiwemo wale waliopata ujauzito wakiwa shule, wanarejea shule.
“Hatuwezi kumzuia mtoto kwenda shule katika dunia ya sasa ya kidijitali. Vilevile, hatuwezi kuendelea na mitaala ya watu wazima inayopitwa na wakati. Tunapaswa kuhakikisha elimu ya watu wazima inajikita kwenye stadi zitakazosaidia wananchi kuishi na kufanya kazi katika karne hii ya teknolojia,” alisema Mhe. Mtaka.
Kwa upande wake, Afisa Elimu ya watu wazima Mkoa wa Njombe, Fadhili Msilu, amesema mkoa wa Njombe unaendelea na utoaji wa Elimu ya Msingi kwa waliokosa (MEMKWA) ambapo kwa sasa kuna wanafunzi 201 wanaopatiwa masomo hayo. Aidha, kwa wale wenye mahitaji maalumu katika shule za msingi na sekondari, idadi imefikia wanafunzi 7,513.
Ameongeza kuwa kwa sasa elimu ya watu wazima hutolewa kwa njia ya kidijitali tofauti na zamani ambapo mtu mzima alilazimika kufika shuleni au kutumia barua kwa njia ya posta. Mfumo huu mpya umeongeza fursa kwa watu walioko kazini au vijijini mbali na shule kuendelea kusoma bila kuathiri shughuli zao za kila siku.
Maadhimisho ya Elimu ya watu wazima kwa mwaka 2025 yamebeba kauli mbiu isemayo: “Kukuza Kisomo Katika Zama za Kidijitali.”
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe