Tarehe 07 Januari 2025,Kituo cha Afya Ihalula kilichopo Kata ya Utalingolo Halmashauri ya Mji wa Njombe, kimepokea gari jipya la kubebea wagonjwa (Ambulance).
Gari hilo limekabidhiwa rasmi na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Deo Mwanyika ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya na kuwahudumia wananchi kwa haraka zaidi wakati inapotokea dharura.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mheshimiwa Mwanyika amesema kuwa gari hilo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa kwa wananchi wa kata ya Utalingolo.
"Tangu ziara yangu ya kwanza nilipofika hapa moja ya changamoto mlizoniambia nakuniomba haswa akina mama ni gari la wagonjwa wa dharura, nilitoa ahadi na diwani wenu amekuwa akinikumbusha mara kwa mara na leo ninafurahi kuwa ahadi imetimia," amesema Mhe.Mwanyika.
Kuhusu matumizi na utunzaji wa gari hilo Mheshimiwa Mbunge amesisitiza gari hilo ni kutumika kwenye kazi iliyokusudiwa.
"Gharama ya gari hili ni shilingi Milioni 250, gari hili ni gari kwa ajili ya shughuli maalumu kama tulivyoelezwa siyo la kutembelea au kuzururia siyo kwa ajili ya kufanya kazi tofauti na mahitaji yake. Hili gari ni la kwenu kwa maana ya kwamba wote tunajukumu la kulitunza," amesisitiza Mhe. Mwanyika.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Mhe. Erasto Mpete amewashukuru viongozi wa Serikali hususani Mhe.Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika kwa kusikiliza kilio cha wakazi wa Kata ya Utalingolo na kuwezesha upatikanaji wa gari hilo na amesisitiza gari hilo kutunzwa ili liweze kudumu na kuwahudumia wananchi kwa muda mrefu.
"Vizazi vyetu na vinavyofuata wanatakiwa wanufaike na hili gari kwa hiyo tuombe ushirikiano baina ya wataalamu na wananchi na mganga mfawidhi wa kituo tunaomba hili gari litunzwe," amesisitiza Mhe. Mpete.
Kwa upande wao wananchi wa Kijiji cha Ihalula walitoa shukrani zao dhati kwa Serikali na Mbunge wao kwa kutambua hitaji lao la muda mrefu na kulitekeleza.
Hafla ya kukabidhi gari hilo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo waheshimiwa madiwani kutoka kata nyingine za Halmashauri ya Mji Njombe.
Gari hilo la wagonjwa litatoa huduma katika kata ya Utalingolo na kata nyingine za jirani kulingana na uhitaji wa eneo husika.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe