Wananchi wa Kijiji cha Uliwa, Kata ya Iwungilo, Halmashauri ya Mji wa Njombe, Oktoba 08,2025 wamepokea habari njema kufuatia mpango wa kufungwa kwa mashine ya kuongeza virutubishi kwenye unga, iliyotolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na mdau wa maendeleo, kampuni ya Sanku.
Mashine hiyo ni miongoni mwa tatu zilizotolewa kwa ajili ya kuchanganya virutubishi muhimu kama madini ya chuma na zinki kwenye unga wa mahindi, na itafungwa katika Kijiji cha Uliwa ili kuwahudumia wananchi kwa lengo la kupambana na utapiamlo na udumavu katika jamii.
Pamoja na taarifa ya uwekaji uwekaji wa mashine hiyo, wananchi pia wamepatiwa elimu ya lishe bora inayolenga kuboresha afya kupitia ulaji wa chakula chenye virutubishi vya kutosha na kuzingatia makundi yote ya vyakula.
Elimu hiyo imetolewa na Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Ndg.Michael Sway, katika mkutano uliofanyika kijijini hapo, ambapo alieleza kuwa mashine hizo zitafungwa katika vijiji vya Uliwa, Utalingolo pamoja na Mtaa wa Ramadhani.
“Kupitia mashine hizi, wananchi watanufaika na unga wenye mchanganyiko wa virutubishi muhimu, hasa madini ya chuma na zinki. Virutubishi hivi husaidia kuongeza nguvu mwilini, kusaidia ukuaji wa mifupa, kulinda afya ya mama mjamzito, na hata kuzuia mimba kuharibika,” alisema.
Aidha, aliwasisitiza wakina mama wajawazito na wale wenye watoto wachanga kuwa miongoni mwa walengwa wakuu wa huduma hiyo, kwa kuwa wao wako katika makundi yanayohitaji virutubishi kwa kiwango kikubwa zaidi kwa ajili ya afya ya mama na mtoto.
Matumizi ya vyakula vilivyoboreshwa kwa virutubishi ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupambana na tatizo la lishe duni na udumavu, hasa katika maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa chakula mchanganyiko unaweza kuwa changamoto kubwa.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe