Hayo yamesemwa na waalimu wa shule mbalimbali katika Halmashauri ya Mji Njombe, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo juu ya wanafunzi wanaoishi na VVU yalioendesha na shirika la watu wanaoishi na VVU Njombe wakishirikiana na Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Mji Njombe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti waalimu hao wamesema kuwa wazazi wengi wamekuwa hawatoi taarifa juu ya afya za watoto wao jambo ambalo limekuwa likiwafanya waalimu kutojua afya za watoto pindi wawapo shuleni.
“Wanafunzi wanaoishi na VVU wanakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo unyanyapaa. Kutokana na kuwa waalimu hususani waalimu wa malezi wanakuwa hawana taarifa sahihi za mwanafunzi. Unaweza ukawa umemwadhibu mtoto kwa kutofika shuleni kumbe alienda kuchukua dawa, lakini huna taarifa mzazi hajakushirikisha chochote na hufahamu lolote. Wakati mwingine tunapokuwa tunataarifa inasaidia hata kuona ni kwa namna gani unamsaidia mwanafunzi husika.”Alisema Herry ambaye ni Mratibu Elimu Kata ya Mjimwema.
Herr aliongezea kuwa kujua afya ya mwanafunzi kunamsaidia mwalimu katika kupanga ratiba ya majaribio na mitihani mbalimbali bila kuingiliana na ratiba za wanafunzi wanaochukua dawa lakini pia kumpatia ruhusa mwanafunzi pindi anapotaka kwenda kuchukua dawa. Aidha taarifa hizo za afya zinawawezesha waalimu kutoa ushauri wa kiafya kwa wanafunzi kwa kuzingatia lishe bora.
Kwa wakati huo huo, Mratibu huyo wa Elimu amewataka waalimu kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na kuacha kujihusisha kimapenzi na wanafunzi kwani jambo hilo ndio limeibua hofu miongoni mwa wazazi kwa kukosa uaminifu na waalimu kutokana na kuwepo na kesi nyingi zinazowahusisha waalimu kuwa na mahusiano ya kimapenzi wa wanafunzi wao na kuwataka waalimu kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wanafunzi kimalezi.
Mwalimu Steven Mwakila ambaye ni mwalimu wa malezi Mpechi Sekondari amewaomba viongozi wa dini kuhubiri maswala ya UKIMWI kwenye nyumba za ibada kwani janga hili sasa limeenda mbali zaidi katika Mkoa wa Njombe na sasa wanafunzi wengi wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo vya ngono jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maambukizi ya VVU.
Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa ni ugumu wa maisha katika ngazi za familia sambamba na wazazi wengi kujihusisha zaidi na shughuli za kimaendeleo na kusahau elimu ya malezi kwa watoto jambo ambalo linapelekea watoto wengi kujiongoza wenyewe kimalezi. Wazazi wamehimizwa kutoa taarifa juu ya afya za watoto wao kwa waalimu badala ya kufanya siri kwani kunadidimiza maendeleo ya mtoto shuleni lakini pia wazazi kuwa karibu na watoto wao kwa kufuatilia maendeleo yao shuleni lakini pia nidhamu za watoto pindi wawapo shuleni badala ya watoto kujiongoza wenyewe na kufanya maamuzi ya maisha yao wenyewe jambo ambalo linawaingiza wengi katika makundi yasiyofaa na kupelekea mmomonyoko wa maadili.
Takwimu zinaonyesha kuwa kwa upande wa Halmashauri ya Mji Njombe, Wanafunzi 229 katika shule za msingi wanaishi na VVU na wanafunzi 62 ikiwa ni katika shule za Sekondari.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe