Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kung’ara katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025, kwa kufanikisha utoaji wa huduma muhimu za lishe kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Afisa Lishe wa Halmashauri Bw. Michael Swai amesema mafanikio makubwa yamepatikana katika viashiria vyote muhimu vya mkataba wa lishe katika kipindi cha robo ya nne 2024/2025.
Bw. Swai ameeleza kuwa utoaji wa elimu na unasihi wa ulishaji wa watoto wachanga na wadogo wenye umri wa miezi 0 hadi 23 ulifanyika kwa mafanikio makubwa, ambapo lengo lilikuwa kuwafikia akina mama 2,484 lakini waliopatiwa elimu hiyo walifikia 3,716, sawa na asilimia 100 ya lengo lililowekwa.
Aidha, huduma ya unasihi katika vituo vya kutolea huduma za afya iliwafikia watu 20,700 ambao ndio walengwa waliopangwa, huku huduma ya utoaji wa vidonge vya kuongeza damu kwa wanawake wajawazito waliokuwa wakihudhuria kliniki nazo zikitolewa kikamilifu kwa wanawake 8,241 sawa na asilimia 100 ya waliotarajiwa.
Katika kuhakikisha watoto wanapata kinga dhidi ya upungufu wa vitamini A, watoto 22,028 wenye umri wa miezi 6 hadi 59 walipatiwa matone ya vitamini A, zaidi ya lengo la awali la watoto 21,110, sawa na asilimia 100 ya utekelezaji.
Kwa upande wa matibabu ya utapiamlo mkali, watoto 5 chini ya miaka 5 walipokelewa katika kipindi hicho, ambapo watoto 4 walipona na mmoja alifariki dunia.
Katika jitihada za kuhamasisha jamii kuhusu lishe bora, Bw. Swai amesema kuwa vijiji na mitaa yote katika Halmashauri hiyo vilifanya maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji, huku ikiripotiwa ongezeko la ushiriki wa wanaume katika shughuli hizo jambo ambalo awali lilikuwa changamoto kubwa katika kampeni za lishe.
Halmashauri ya Mji Njombe bado inaendelea na juhudi za makusudi kukabiliana na changamoto za udumavu, uzito pungufu na uzito uliozidi kwa watoto chini ya miaka mitano. Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia robo ya nne ya mwaka 2024/2025, kiwango cha udumavu kimefikia 42.4%, uzito pungufu 9.4%, na uzito uliozidi 9.0%.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe