Halmashauri ya Mji Njombe imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni mia mbili thelathini na tisa laki tisa na themanini elfu kwa vikundi 24, vikundi 08 vikiwa ni kwa vijana na vikundi 16 vya wanawake hii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali ambapo Halmashauri imeweza kutenga asilimia kumi za mapato yake ya ndani kwa ajili ya zoezi hilo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya hundi ya mfano Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Romanus Mayemba ameipongeza Halmashauri kwa jinsi ambavyo imeweza kufanya usimamizi na kuhakikisha kwamba maagizo ya Serikali ya utoaji mikopo bila riba yanatekelezwa katika kila robo na kuwafikia walengwa kwa wakati.
“Niwapongeze wale wote mliobahatika kupata mikopo.Fedha za mikopo zinazotolewa zinajumuisha asilimia kumi ya mapato ya ndani pamoja na marejesho. Unaporejesha mikopo unatoa fursa kwa vikundi vingine vyenye sifa kuweza kukopa lakini pia unajijengea sifa ya kukopeshwa kwa mara nyingine. Tuzingatie urejeshaji wa mikopo kwa wakati. Tunapokwenda kutumia mikopo tuwe na uhakika wa kuirejesha na hii itatusaidia kusukuma maendeleo kwenye Halmashauri yetu. Uaminifu ni jambo la msingi sana. Alisema Mayemba
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi. Illuminatha Mwenda amesema kuwa Halmashauri imeweza kutoa mikopo mingi kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani jambo ambalo linapelekea ongezeko la utoaji mikopo kila wakati na hivyo amewataka Wananchi kuhakikisha kuwa wanakuwa wachangiaji wazuri wa mapato na kuwa wasimamizi kwa kuhakikisha kuwa hakuna upotevu wa mapato kwani mafanikio hayo ni kutokana na makusanyo ya mapato ya ndani kuwa mazuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti baadhi ya wawakilishi wa vikundi hivyo wameipongeza Halmashauri kwa jitihada hizo na wameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufanya marejesho na kupata fursa ya kuweza kukopeshwa tena.
Kwa upande wake Donas Innocent Kayombo mwakilishi kutoka kikundi cha Vijana Melinze amesema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo vijana kwenye uundaji wa vikundi ni ukosefu wa shughuli ya pamoja jambo linalopelekea vijana wengi kushindwa kujiunga kutokana na kuwa kila kijana anakuwa na shughuli yake ya kujiongezea kipato na hivyo kuiomba Serikali kuweza kuboresha miongozi hiyo ili kasi ya ukopaji kwa vijana iwe kubwa.
“Tulikuwa tunasikia mitaani kuhusu mikopo. Tukaamua kuunda kikundi. Tuliomba milioni kumi na tumepata kadri tulivyoomba na tunakwenda kuinuka kiuchumi.”Alisema Kayombo
Naye Rehema Nyezi mwakilishi kutoka kikundi cha wanawake amesema kuwa wanaishukuru Halmashauri kwani wameweza kupatiwa mkopo kadri walivyoomba na amesema kuwa lengo lao ni kwenda kuanzisha kilimo cha parachichi na kuendeleza mradi wa ufugaji kuku na wameahidi kwenda kufanyia kazi fedha hizo ili waweze kuzirejesha kwa wakati.
Ikumbukwe kuwa kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 Halmashauri imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia tisa arobaini laki nane na themanini kwa vikundi 96 ambapo 72 vya wanawake 22 vijana na 2 walemavu ikiwa ni mapato ya ndani ya Halmashauri na fedha za marejesho. Rai imeendelea kutolewa kwa watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya ambapo kwa sasa kumekuwa na mabadiliko ya idadi ya wanaojiunga ambapo hata mlemavu mmoja anaweza kuomba na kupatiwa mkopo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe