Halmashauri ya Mji Njombe imekabidhi trekta lenye thamani ya shilingi milioni 75 kwa muungano wa vikundi 5 vijulikanavyo kama Lusitu Agribusiness Group ikiwa ni mkopo utokanao na asilimia 10 za mapato ya ndani ambapo hutumika kutoa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi trekta hilo Mbunge wa Jimbo la Njombe Kusini Edward Mwalongo amesema kuwa anaipongeza Halmashauri kwa ubunifu huo ambao utaleta chachu kwa jamii kujiunga katika vikundi na kuchochea maendeleo katika jimbo hilo.
“Halmashauri ya Mji Njombe imewezesha wananchi kupata kitendea kazi kupitia mikopo ya asilimia kumi. Niwaombe kuwa watunzaji wa trekta hili na kuhakikisha kuwa mkopo unarejeshwa ili tuweze kukopesha na wengine. Wito wangu ni kwa wale wote waliokopeshwa fedha za asilimia kumi za mapato ya ndani kuhakikisha kuwa zinarudishwa kwa wakati ili waweze kupata fursa ya kuongezewa mikopo na kukopesha vikundi vingine” Alisema Mwalongo
Wakizungumza kwa wakati tofauti tofauti Katibu wa kikundi hicho Benson Mgaya na Mwenyekiti wa Kikundi Claudia Mhenga wamesema kuwa trekta hilo litarahisisha uendeshaji wa shughuli za kilimo kwa wakati kwani changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili ni upatikanaji wa trekta kwa ajili ya kulima mashamba na kubeba mazao jambo ambalo awali lilikuwa linasababisha kushindwa kulima kwa kiasi kikubwa na wakati mwingine kupelekea mazao kuoza na kuharibiwa na mvua kutokana na changamoto ya ubebaji wa mazao wakati wa uvunaji.
“Tulikuwa tukiwaza wapi tutapata mkopo wa trekta kwa ajili ya kuturahisishia shughuli zetu. Tunaishukuru Halmashauri kwamba ilikubaliana na wazo letu. Sasa tunaenda kufanya kazi. Alisema Claudia Mhenga Mwenyekiti wa Kikundi”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi. Illuminatha Mwenda amesema kuwa kutokana na kuwa kikundi hicho kimeonesha nia ya dhati ya kujikwamua kiuchumi kwa kushiriki katika shughuli za uzalishaji Halmashauri imewaunga mkono kwa kuwapatia lita mia moja za mafuta ili kuweza kuanzia shughuli zao.
Katika kila robo mwaka Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kutekeleza maagizo ya Serikali kwa Kuhakisha kuwa asilimia kumi zitokanazo na mapato ya ndani zinatengwa kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe