Halmashauri ya Mji Njombe imetoa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa Shule 8, Sekondari Shule 4 na Msingi 4 ikiwa ni sehemu ya motisha kwa ufaulu mzuri katika mitihani ya Kitaifa ya kidato cha nne na cha saba ambapo kiasi cha shilingi laki tano kimetolewa kwa kila shule.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amesema kuwa licha ya kuwa Waalimu hao wamekuwa wakisimamia taaluma katika Shule zao pia wamekuwa ni msaada mkubwa katika kusimamia maendeleo kwenye Shule hizo.
“Tumeona kazi mnayofanya ni kubwa na hatungependa kuwaacha hivi. Hii ni asante kwa kazi kubwa mnayofanya ya kusimamia taaluma kwenye maeneo yenu. Kwa bajeti ijayo tumeona tutenge fedha ili kuendelea kuleta hamasa kwa waalimu kufanya vizuri zaidi. Tunaamini kazi mnayofanya ni kubwa na sisi tupo nyuma yenu.”Alisema Mwenda
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Huduma za Jamii Halmashauri ya Mji Njombe ambaye ni Diwani wa Kata ya Luponde Ultrick Msemwa amesema kuwa mchango wa waalimu katika Halmashauri ni mkubwa kwani wanachangia katika ufaulu ndani ya Mkoa wa Njombe na pia kuipatia heshima Halmashauri.
“Tuendelee kuitetea nafasi ya kufanya vizuri na tuendelee kufanya vizuri zaidi na kupandisha ufaulu katika Shule zetu. Sisi kama wawakilishai wa Wananchi ambao watoto wetu ndio mnaowafundisha tumejitahidi kwa kadri inavyowezekana kwa chochote kilichopo ndani ya Halmashauri na ninyi muweze kupata.Niendelee kuwatia moyo na kuwaambia kuwa licha ya kuwepo na mazingira mbalimbali kwenye shule, Baraza la Madiwani na Halmashauri inaendelea kupambana siku hadi siku kuhakikisha kuwa inaboresha mazingira ya kufanyia kazi ikiwa ni ujenzi wa madarasa na ofisi na ujenzi wa nyumba za waalimu ili mazingira ya ufanyaji kazi yawe rafiki.”Alisema Mheshimiwa Msemwa.
Akizungumza kwa niaba ya Waalimu waliopatiwa motisha Mkuu wa Shule ya Sekondari Mpechi Brown Kiswaga amesema kuwa wanaishukuru Halmashauri kwa kujali na kuona umuhimu wa kazi wanayofanya na kusema kuwa jukumu walilonalo ni kuhakikisha kuwa mwakani wanafanya vizuri zaidi na idadi ya shule zitakazokuwa zimefanya vizuri kuwa nyingi zaidi ya sasa kwa kuendelea kuhamasishana.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe