Halmashauri ya Mji Njombe imeweza kutekeleza kikamilifu agizo la Serikali kwa kuzitaka Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike ambapo kiasi cha shilingi milioni kumi kiliweza kutumika kwa ajili ya ununuzi wa taulo hizo kwa Shule za Sekondari.
“Kwa kuanza Halmashauri imeweza kutenga kiasi cha Shilingi milioni kumi ambapo Halmashauri imeweza kununua maboksi 260 ambapo kila boksi lina paketi 24 na kufanya jumla ya taulo sitini na mbili elfu na mia nne ambazo zitagawiwa kwa Shule zote 24 zenye wanafunzi wa kike katika Halmashauri ya Mji Njombe.” Alisema mratibu wa mpango ngazi ya Halmashauri Joyce Ngata.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano kwa wanafunzi wa kike Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri amesema kuwa kwa sasa taulo za kike limekuwa si jambo la aibu kama ilivyokuwa zamani na imekuwa ni sehemu ya usafi kwa mtoto wa kike na ameipongeza Halmashauri kwa kutekeleza maagizo hayo.
“Serikali pia imeweza kuliwekea mkazo na Halmashauri imeweza kulitekeleza kwa kasi kubwa. Hii ikawe ni utunzaji bora wa afya za wanafunzi wa kike waelekezwe namna nzuri ya uhifadhi mara baada ya matumizi ili zisisababishe uchafuzi wa mazingira.”Alisema Mkuu wa Wilaya
Aliendelea kusema “Tuwasaidie watoto wakike wasiweze kupoteza masomo. Kuna kipindi watoto wa kike wanashindwa kwenda shuleni kwa kukosa hifadhi nzuri.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbeyela Valeno Kitalika amesema kuwa Taulo hizo zitakuwa msaada mkubwa kwa Wanafunzi wa kike kwani kuna wazazi wanoshindwa kumudu gharama za kununua vifaa hivyo kupelekea watoto wa kike kushindwa kuhudhuria shuleni katika kipindi wawapo katika mizunguko yao.
Wakipokea taulo hizo baadhi ya wanafunzi kutoka shule ya Sekondari Agness Trust Tumaini Maheve na Sayuni Festo Mhagama kutoka Shule ya Sekondari Maheve wamesema kuwa taulo hizo zitawasaidia kuweza kuhudhuria vipindi vyote vya darasani na kuwafanya kuwa huru zaidi.
Halmashauri inaendelea na utaratibu wa kutenga fedha na kuhakikisha kuwa katika kila mwaka taulo za kike zinanunuliwa kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya Msingi mpaka Sekondari.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe