Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea na utaratibu wa kuwapatia misaada makundi ya watu wenye mahitaji maalumu ambapo kiasi cha shilingi milioni moja laki sita kimetolewa kwa kikundi cha wazee 8 kutoka katika Kata ya Uwemba Kijiji cha Njoomlole kwa ajili ya kuwasaidi wazee hao kwenye shughuli za kujiongezea kipato na kuboresha makazi yao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo Afisa Ustawi wa jamii Halmashauri ya Mji Njombe Petro Mahanza amesema kuwa Kitengo cha ustawi wa jamii kimeendelea kuwashika mkono watu wenye mahitaji mbalimbali na kuwa sauti kwa wasio na sauti wakiwemo wazee,watoto na watu wenye ulemavu.
“Kilio chenu kimesikika kulingana na mahitaji yenu. Mkurugenzi wa Halmashauri ametoa kiasi cha shilingi milioni moja laki sita na kila mzee atapata kiasi cha shilingi laki mbili.”Alisema Mahanza
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Uwemba Jactan Mtewele amekitaka kikundi hicho cha wazee kijulikanacho kama TWITANGE MAGUFULI kuzitumia fedha hizo kulingana na mahitaji waliyoyaombea na kuwa mfano mzuri.
“Yapo mahitaji mbalimbali ambayo wazee mliweza kuyaainisha katika andiko lenu ambalo mlinipatia.Tukumbuke kuwa andiko lenu lipo katika Ofisi yangu,Ofisi ya Afisa Maendeleo wa Kata, Ofisi ya Mtendaji Kata na Katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri. Wapo walioomba fedha kwa ajili ya kufuga kuku, kupanda parachichi, na shughuli mbalimbali.Itashangaza siku Mkurugenzi akitaka kuwatembelea na kuona shughili mlizofanya mara baada ya kupewa fedha na tukafika tusione kilichofanyika.Niwasihi chochote mtakachoenda kukifanya kiende sehemu sahihi”Alisema Diwani Mtewele.
Maafisa Maendeleo kutoka Halmashauri ya Mji Njombe Christina Tengay na Afisa Maendeleo Kata ya Uwemba Flora Kapinga wao wamesema kuwa licha ya kuwa wazee hao wamepatiwa fedha hizo wataendelea kuwasimamia ili kufanikisha shughuli zao na kuwashirikisha wataalamu wa ugani na mifugo kwa wazee waliopanga kufanya shughuli za kilimo na mifugo.
“Tunachokiomba ni utekelezaji. Sisi kama wataalamu huwa tunakwenda kuomba fedha hizi kwa Mkurugenzi inabidi mkawe chachu kwa wengine wenye mahitaji. Sisi tunatamani tuone maendeleo yanapatikana kwa sababu fedha hiyo inakidhi hitaji la kila mmoja kwa kadri alivyoiombea.”Christina alisema
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa fedha hizo baadhi ya wawakilishi kutoka kikundi hicho cha wazee akiwemo Illuminatha Mlowe, Mikaela Samlongo ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi cha TWITANGE MAGUFULI ametoa shukrani zake kwa uongozi mzima wa Halmashauri na kuahidi kufanya kazi kwa kadri ya mahitaji yao na amewataka wazee wengine kuiga mfano huo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe