Kuelekea maadhimisho ya siku ya Usafi wa mazingira Duniani Halmashauri ya Mji Njombe imezindua wiki ya maadhimisho hayo kwa kufanya usafi wa mazingira katika Mtaa wa Idudilanga, Kata ya Njombe Mjini, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kushiriki katika utunzaji wa mazingira.
Akizungumza mei 31 ,2025 wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Njombe, Nelson Mlwisa, aliwataka wananchi kuwa na tabia endelevu ya kufanya usafi katika maeneo yao ili kuimarisha afya ya jamii na kuzuia magonjwa ya mlipuko yanayochangiwa na uchafuzi wa mazingira.
“Ni muhimu kila mwananchi kuwajibika katika kutunza mazingira Usafi wa mara kwa mara huleta mandhari safi, salama na hupunguza hatari ya milipuko ya magonjwa kama kipindupindu,” alisema Mlwisa.
Zoezi hilo la usafi lilihusisha wananchi wa Mtaa wa Idudilanga pamoja na watumishi wa halmashauri, ambapo walifanya usafi katika maeneo ya makazi, barabara na mitaro ya maji taka.
Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani hufanyika kila mwaka ifikapo Juni 5, yakilenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na kuchukua hatua dhidi ya uharibifu wa mazingira, hususan matumizi holela ya plastiki.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni: "Mazingira yetu na Tanzania ijayo tuwajibike sasa, dhibiti matumizi ya plastiki."
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe