Halmashauri ya Mji Njombe imeshika nafasi ya kwanza kwa upande wa Halmashauri za Miji kwa kuibuka kidedea kwenye mashindano ya Usafi na Mazingira Nchini na kukabidhiwa zawadi ya trekta na tuzo maalumu huku sekondari ya wavulana Njombe ikishika nafasi ya kwanza kwa shule za sekondari za serikali nchini na kukabidhiwa zawadi ya tuzo maalumu na pikipiki.
Hayo yamebainishwa leo wakati wa kuwakabidhi zawadi washindi wa mashindano hayo ikiwa ni sambamba na kuhitimisha kilele cha wiki ya Usafi na Mazingira Kitaifa ambapo mgeni rasmi katika Halfa hiyo alikuwa Waziri Mkuu wa Nchi Mhe. Kassim Majaliwa Kassim hafla iliyofanyika katika ukumbi wa wa Julius Nyerere- Mipango jijini Dodoma.
Akihutubia katika hafla hiyo Waziri Mkuu amewataka Wakurugenzi nchini kuhakikisha kuwa kufikia Desemba 31 kila Halmashauri iwe imefikia lengo la kuhakikisha kuwa kila familia na jamii inakuwa na vyoo bora na vya kisasa kwani vitasaidia kupunguza uwezekano wa kutokea magonjwa ya milipuko ambayo yanaweza kusababishwa na ukosefu wa vyoo bora.
“Niwatake muhakikishe Maofisa Afya wanawezeshwa katika kutoa elimu kwa Wananchi ili suala la ujenzi wa vyoo bora na vya kisasa litekelezeke kwa ufanisi mkubwa na Maofisa afya muhakikishe mnafanya Ukaguzi wa mara kwa mara ili jambo hili liweze kufanikiwa.”alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema katika awamu ya pili ya Kamapeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira wizara yake imejipanga kuhakikisha asilimia 75 ya kaya nchini zinakuwa na vyoo bora na kuondoa kaya ambazo hazina vyoo kabisa ambapo kupitia kampeni hiyo iliyoanza imewezesha kupunguza idadi ya kaya zisizokuwa na vyoo kutoka asilimia 9.5 (2015) mpaka kufikia 3.8 (2018).
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa zawadi hizo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga amesema kuwa ushindi huo kwa upande wa Halmashauri yake inaonesha ni kwa jinsi gani wananchi wa Mkoa wa Njombe wanakerwa na swala la uchafu wa Mazingira na amesema kuwa zawadi hizi zitaenda kuleta chachu ya utunzaji Mazingira kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki ipasavyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amesema kuwa ushindi huo ni wa halmashauri kwa ujumla kwani kila mtu amehusika kwa namna moja au nyingine katika kuhakikisha kuwa ushindi huo unapatikana na amewaomba wananchi kuendelea kuchangia tozo za taka kwa wingi kwani mafanikio sio kitu cha kiurahisi.
Mkoa wa Njombe umeweka heshima kwa upande wa Usafi na Mazingira ambapo Halmashauri ya Mji Njombe na Halmashauri ya wilaya ya Njombe zimekuwa za kwanza Kitaifa kwa upande wa Halmashauri za Miji na wilaya,na kufanikiwa kutoa vijiji bora na shule bora ya sekondari ya serikali Njombe.
Ikumbukwe kuwa kwa awamu ya tatu mfululizo Halmashauri ya Mji na Wilaya ya Njombe zimekuwa mabingwa wa mashindano hayo na kuibuka na zawadi nono za trekta na magari ambapo rai imetolewa kwa Halmashauri nyingine kuiga mfano wa Halmashauri ya Mji Njombe na Wilaya ya Njombe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe