Halmashauri ya Mji Njombe leo imesaini mikataba na vikundi vilivyopatiwa mikopo ya asilimia kumi ikiwa ni miongoni mwa hatua muhimu zilizopo kwenye miongozo ya uchukuaji wa mikopo hiyo.
Akizungumza wakati wa zoezi la utiaji saini wa mikataba hiyo Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri Enembora Lema amesema kuwa licha ya kuwa vikundi vimekuwa vikijitahidi kushiriki katika shughuli za ujasiriamali bado kumekuwa na changamoto ya vikundi vya wanawake kwani wengi wao wamekuwa wakichukua fedha na kugawana badala ya kuziingiza kwenye shughuli za ujasiriamali jambo ambalo limekuwa likipelekea kuchelewa kwa marejesho.
“Kila kikundi kina shughuli ambayo imekiwezesha kupata mkopo kwa kadri ya maombi yenu. Baada ya wiki mbili tutapita katika kila kikundi na kuhakiki shughuli ambazo mmeelekeza fedha hizo. Kwa wale ambao mnamawazo ya kwenda kugawana fedha hizo tuache mara moja” Alisema Afisa Maendeleo
Naye Afisa Maendeleo anayeshughulikia mikopo Christina Daniel amevitaka vikundi hivyo kuhakikisha kuwa wanakuwa na utunzaji sahihi wa taarifa za kikundi hususani taarifa za fedha na kuhakisha kuwa wanavikundi wanashiriki ipasavyo katika vikao vya kikundi ili kujenga uelewa wa pamoja na kujua yale yanayoendelea ndani ya kikundi husika.
“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanavikundi kutohudhuria kwenye vikao hili jambo sio zuri kwani kama kikundi kuna mambo inabidi kukubaliana kwa pamoja. Wanufaika wengi wa mikopo hii ni wa Kata za Mjini inawezekana baadhi mmepanga. Inapotokea umehama toa taarifa kwa wanakikundi wengine”Alisema Christina
Katika hatua nyingine Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika akizungumza na wanufaika wa mikopo hiyo mara baada ya kuwatembelea na kushuhudia zoezi la ujazaji mikataba. Mbunge huyo amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia kumi kuhakikisha kuwa wanarejesha mikopo kwa wakati ili iweze kuwanufaisha na wengine.
“Njombe tumeweza kutoa bilioni kwenye mikopo.Hii inaashiria kuwa uchumi wetu umeimarika na utaratibu wa utoaji asilimia kumi unatekelezwa.Tunatoa pongezi kwa wafanyabiashara na walipa kodi wa Njombe. Wao ndio walioleta hizo fedha.Tunazidi kuiomba Serikali iendelee kuweka utaratibu mzuri zaidi ili kuweza kufikia malengo kwenye hii mikopo.Alisema Mwanyika
Aidha Mwanyika ameahidi kuvitembelea vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo na kutoa fedha kiasi cha shilingi laki tano kwa kila kikundi kwa jumla ya vikundi vitatu vitakavyokuwa vimefanya vizuri ikiwa ni zawadi na motisha kwao kuendelea kuongeza bidii kwenye shughuli za kiuchumi.
Ikumbukwe kuwa mnamo tarehe 15 mwezi Novemba Halmashauri ilikabidhi hundi ya shilingi bilioni 1.2 kwa vikundi 116 vya vijana,wanawake na watu wenye ulemavu katika tamasha la Njombe ya Mama Samia lililoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe,ikiwa ni utekelezaji wa mwongozo wa Serikali wa kuzitaka Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kila robo kutoa mikopo iiyo na riba kwa vmakundi hayo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe