Wakizungumza katika Mkutano wa Baraza la Waheshimiwa Madiwani wakati wa kujadili taarifa ya Kamati Mipangomiji na Mazingira Madiwani Halmashauri ya Mji Njombe wameipongeza kamati hiyo kwa hatua waliochukua ya kutekeleza maagizo ya baraza lililopita kwa kuwatoa wafanyabiashara katika maeneo yasiyo rasmi ikiwemo pembezoni mwa barabara na kutokufurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Wilaya ya kuwarejesha tena wafanyabiashara katika maeneo hayo licha ya vikao na matangazo kutolewa ya kuwaelekeza maeneo ya kufanyia biashara na kusababisha kukinzana kwa majukumu
Wakioneshwa kutoridhishwa kwa maamuzi yaliyofanywa baadhi ya Madiwani Filoteus Mligo Diwani wa Kata ya Lugenge ,Ultrick Msemwa Diwani wa Kata ya Luponde na Nestory Mahenge Diwani wa Kata ya Mji Mwema wamesema kuwa Halmashauri ya Mji Njombe ipo katika hatua za awali za kupeleka mapendekezo ya kuipandisha hadhi Halmashauri na hivyo uwepo wa Wafanyabishara barabarani ni mojawapo ya vikwazo vitakavyopelekea kushindwa kufikia malengo hayo.
Madiwani hao kwa pamoja waliafiki maeneo ambayo si rasmi kutokuendelea kutumika kwa ajili ya kufanyia biashara hizo na wamewataka Watumishi kuendelea kusimamia zoezi la usafi na kumwomba Mkuu wa Wilaya kuchukua hatua za haraka ili kuweza kunusuru Mji wa Njombe na hali ya uchafu iliyopo sasa na ongezeko la wafanyabiashara barabarani.
“Hatuwezi kuwa na Mji wa kuuza mali mbichi kila mahali.Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa soko.Lakini wafanyabishara waliopo sokoni nao wanatoa malimbichi na kuuza nje ikiwemo barabarani.Inabidi tusimamie ipasavyo usafi wa mji na kutowaendekeza wale wote wanaokiuka kanuni za usafi wa mazingira.”Alisema Diwani
Awali Akiwasilisha salamu za Serikali Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri amewataka Waheshimiwa Madiwani kufanya kazi kwa bidii na kwa malengo na kuhakikisha kuwa usimamizi wa miradi unafanyika kwa ufanisi mkubwa ili adhma ya Serikali iweze kutimia.
Aidha Mkuu wa Wilaya amesema kuwa licha ya uwepo wa Maagizo mbalimbali yanayotolewa katika vikao mbalimbali ni vyema utekelezaji wa maagizo hayo ukafanywa kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu na bila uonevu ili haki iweze kutendeka kwa kila Mwananchi.
Agenda nyinginge iliyoweza kuzua mjadala ni pamoja na uwepo wa shule kwa ajili ya watoto wenye vipaji ya Utalingolo hoja iliyoibuliwa na Diwani wa Kata ya Matola Edwin Mwanzinga ambapo kwa amesema kuwa uwepo wa shule hiyo utasababisha kushuka kwa ufaulu kwani watoto wenye ufaulu wa juu wanatakiwa kuchanganyika na wenye ufaulu wa kati na wa wastani ili kuweka mchanganyiko mzuri katika kujifunza na kuomba Idara ya elimu kuwapeleka wanafunzi kulingana na ufaulu wao.
“Mimi sikubaliani na uwepo wa shule ya watoto wenye vipaji maalumu.Katika Kata yangu wale wote wenye ufaulu wa A mmewachukua tumebaki na wenye ufaulu wa B na C.Mazingira ndio hupelekea wakati mwingine mtoto kushindwa kufanya vizuri. Mimi nakubaliana na ubadilishanaji wa Wanafunzi. Wanafunzi wa Matola wasome Utalingolo na Utalingolo au Kata nyingine wasome Matola. Lakini utaratibu wa ufaulu wa A wawe na shule yao maalumu huo utasababisha Halmashauri yetu ishindwe kufanya vizuri kwani watoto hao wanatakiwa kuchangayika ili wale wenye ufaulu mdogo waweze kujifunza kwa wenzao wenye ufaulu mkubwa. Alisema Mwanzinga
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Erasto Mpete ambaye ni Diwani wa Kata ya Utalingolo amesema kuwa lengo la uanzishaji wa shule hiyo ni kuleta hamasa na ushindani kwa wanafunzi ambao wanataraji kuingia kidato cha kwanza ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao lakini si kushusha ubora wa elimu.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Halmashauri Romanus Mayemba ameipongeza Halmashauri kwa kuendelea kusimamia mapato ambapo kufikia mwezi machi Halmashauri imeweza kukusanya mapato kwa asilimia 96.3 ya lengo na hivyo kuhimiza usimamizi zaidi ili lengo liweze kutimia huku ikiwa imesalia miezi miwili kufunga mwaka wa fedha.
Halmashauri ya Mji Njombe ipo katika hatua za awali za kufanikisha vigezo vitakavyoiwezesha Halmashauri hiyo kupanda hadhi kutoka kuwa Mji na kuwa Manispaa huku changamoto kubwa ikiwa ni uwepo wa Wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo ambayo si rasmi jambo linaloharibu mandhari ya Mji na kuifanya Halmashauri kushindwa kukidhi vigezo katika mashindano ya usafi na mazingira na hivyo kupoteza sifa yake ya usafi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe