Na,Ichikael Malisa.
Katika juhudi za kuboresha mazingira ya huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) Serikali kupitia Mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF ilitekeleza mradi wa zaidi ya Shilingi Milioni 173, zilizotumika kujenga jengo la mama na mtoto lenye chumba maalum cha kuhudumia watoto njiti katika hospitali ya Mji Njombe(kibena).
Uwepo wa wodi hiyo maalumu umetajwa kuwa sehemu ya mafanikio ya utoaji wa huduma bora kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati katika hospitali ya Mji Njombe (Kibena).
Akitoa taarifa ya huduma za watoto njiti kwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya watoto Njiti duniani Tarehe 17 Novemba 2024 ,Dr.Rehema Omari ameeleza kuwa hali ya chumba cha awali cha watoto njiti katika Hospitali ya kibena ilikuwa haikidhi mahitaji.
"Awali tangu kuanza kwa kitengo hiki mwaka 2006 kulikuwa na chumba kimoja tu, lakini sasa tumepata jengo jipya la kisasa lina vyumba vinne tofauti, ikiwa ni pamoja na wodi ya kawaida, chumba cha kuhudumia watoto wenye magonjwa ya kuambukiza (isolation), chumba cha Kangaroo Mother Care, na chumba cha uangalizi maalum (HDU)."Alisema.
Kitengo hiki kimeleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa kutoa elimu kwa jamii ,wazazi na walezi ya namna ya kuwasaidia watoto njiti kuishi.
Jengo jipya la mama na mtoto lenye chumba maalumu cha watoto njiti lilianza kutoa huduma Januari 2024 na kufikia mwezi Oktoba 2024, jumla ya watoto njiti 112 wamepatiwa huduma na wote wanaishi hatua inayodhihirisha maendeleo makubwa katika kitengo hicho.
Wananchi wa Halmashauri ya Mji Njombe wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini uhai wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa kuhakikisha mazingira yakutolea huduma yanakuwa bora na ya kisasa.
Hospitali ya Mji Njombe Kibena, ikitajwa kuwa mfano bora wa utoaji wa huduma za afya kwa watoto njiti.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe