Idara ya Afya Halmashauri ya Mji Njombe kupitia mratibu wa TFDA wa Halmashauri wametoa mafunzo kwa Watendaji wa Mitaa na wafanyabiashara wa chakula na vipodozi lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya chakula, dawa na vipodozi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Njombe Dkt. Thomas Samwel Ndalio amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuelezea taratibu sheria na kanuni za Mamlaka ya Chakula na Dawa tozo zinazotumika, haki na wajibu wao katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria za mamlaka ya chakula dawa na vipodozi zinatekelezwa ipasavyo.
“Kumekuwa na changamoto wakati wa kusimamia sheria hizi za TFDA. Changamoto hii ni kwa wale waliokasimiwa madaraka ya kusimamia sheria (Halmashauri) pamoja na Wafanyabishara. Wafanyabiashara wengi hawaelewi tozo wanazotozwa wanatozwa kwa mujibu wa sheria zipi na ndio maana leo tumeamua tuwapatie elimu ili wawe na uelewa wa pamoja lakini pia tunaamini watakuwa waalimu bora kwa wafanyabiashara wengine.”Alisema Ndalio
Akizungumzia manufaa ya mafunzo hayo Mtendaji wa Mtaa wa Mpeto Agnes Flowin Mbilinyi alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao na yanafaa kuwa endelevu.
“Nimejifunza vitu vingi sana hususani kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara za vyakula, dawa na vipodozi. Kwa sasa itakuwa rahisi kufanya kazi ya ukaguzi kwani tayari nimetambua wajibu wangu katika kusimamia sheria za Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi ninawaomba wafanyabishara kuhakikisha kuwa wanafuata sheria ipasavyo ili kuepuka kuchukuliwa hatua pindi wanapokwenda kinyume na sheria.”Alisema Mtendaji huyo.
Kwa upande wake mmoja wa washiriki katika mafunzo hayo Happines Chengula ambaye ni Mfanyabiashara wa bidhaa za vyakula Katika Kata ya Mjimwema alisema kuwa mafunzo hayo yamemjengea uwezo wa kuhakikisha kuwa bidhaa zake zinakuwa na nembo ya ubora TBS na zimethibitishwa na Mamlaka ya chakula na dawa TFDA Ili kulinda afya ya mlaji.
Julius Kahogo ambaye ni mfanyabiashara wa bidhaa za vyakula na vipodozi Mjini Njombe alisema kuwa watendaji wamepewa majukumu ya kusimamia sheria lakini ni vyema busara kutumika na kuhakikisha elimu inatolewa zaidi.
“Zipo kaguzi ambazo huwa zinafanyika lakini Watendaji wamekuwa hawafanyi ipasavyo. Watendaji wengi wamekuwa wakifanya ukaguzi kwa lengo la kukusanya mapato lakini sio kutoa elimu. Wakati mwingine sio kila mtu anakuwa na ufahamu wa jambo ni vyema ukamuelimisha mtu kwanza. Leo kila mtu amepata elimu na mipaka ya kazi kati ya watendaji na wafanyabiashara imeelezwa vizuri.”Alisema
Wafanyabiashara hao wameiomba Halmashauri kupitia Mratibu wa TFDA kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanakuwa endelevu na kuhakikisha kuwa taarifa inafikia wafanyabiashara wengi zaidi ili kwa kipindi kingine waweze kuhudhuria kwa wingi.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe