Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) nchini Tanzania, akiambatana na Msajili wa Bodi ya Maziwa, Prof. Msalya, pamoja na Mratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa kwa kuzingatia Mabadiliko ya Tabianchi, amefanya ziara katika Halmashauri ya Mji Njombe kufuatilia maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo.
Ziara hiyo ilianza kwa kutembelea Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, kisha Kiwanda cha Kusindika Maziwa cha Kends Milk Factory kilichopo Mtaa wa Ngalanga. Hatua ya mwisho, tarehe 15 Agosti 2025, ilikuwa kukutana na wafugaji wa Kijiji cha Igominyi, hususan kikundi cha Muungano, ambacho kimenufaika na mpango wa “Kopa Ng’ombe, Lipa Ng’ombe wa Maziwa” unaolenga kusaidia kaya maskini.
Mkurugenzi wa IFAD alieleza kuridhishwa na juhudi za Halmashauri ya Mji Njombe katika kuwezesha jamii, akisisitiza kuwa mradi huo utaleta mageuzi chanya kwenye sekta ya maziwa na kuongeza kipato cha wananchi. Aidha, alifurahishwa na mapokezi kutoka kwa wafugaji na kuahidi kutoa fedha kusaidia utekelezaji wa mradi huo.
Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa kwa kuzingatia Mabadiliko ya Tabianchi (Climate Smart Dairy Transformation Project – C-SDTP) unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo IFAD, OPEC, French Development Agency, Green Climate Fund, Heifer International na BEN.
Lengo kuu la mradi ni kuboresha njia za kujikimu kimaisha, kuinua hali ya lishe katika kata masikini za wafugaji, na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wafugaji maskini.
Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 katika Halmashauri 22 zilizopo kwenye Mikoa 8 ya ushoroha wa uzalishaji wa maziwa Tanzania Bara na Mikoa 5 ya Tanzania Visiwani. Thamani ya mradi ni Dola za Marekani 18,783,840 (sawa na TZS 47,282,728,240).
Katika Mkoa wa Njombe, utekelezaji utafanyika katika Halmashauri ya Mji Njombe, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe