Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi leo imetembelea Halmashauri ya Mji Njombe lengo ikiwa ni kujifunza na kupata uelewa wa pamoja juu ya jitihada wanazofanya katika kufanikisha maswala ya usafi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu amesema kuwa wameona ni vyema kutembelea Halmashauri zinazofanya vizuri katika swala la usafi wa mazingira kwani kupitia elimu watakayoipata itawasaidia wao kuboresha mapungufu waliyonayo na kuwawezesha kufanya vizuri zaidi.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na matumizi ya sheria ndogo za Halmashauri na matumizi yake, njia bora za ukusanyaji na uhifadhi taka, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kutupa taka, viwango vya ukusanyaji ushuru wa taka na njia zitumikazo kuhamasisha wananchi kuchangia tozo za taka.
Kaimu Afisa Usafi na Mazingira Halmashauri ya Mji Njombe Ndg. Steven Ndonde amesema kuwa Halmashauri iliona ni vyema kufuta maeneo ambayo yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya shughuli za utupaji taka (VIZIMBA) kwani kwa kiasi kikubwa vilikua vinachangia kuchafua mazingira kwa kufanya taka kusambaa hovyo mitaani na badala yake Halmashauri ikaanzisha utaratibu wa kupitisha magari katika mitaa na kukusanya taka jambo ambalo limekua na manufaa makubwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga amesema kuwa iwapo wanasiasa watakubaliana juu ya utaratibu mzuri wa shughuli za uzoaji taka na usafi wa mazingira zoezi hilo hufanyika kwa ufanisi mkubwa bila malumbano
“Inabidi mtambue kuwa tatizo kubwa tupo nalo sisi wanasiasa tunapokubaliana jambo inakuwa rahisi kwa watendaji tunaweza kukubaliana juu ya gharama za uzoaji taka lakini tunapopeleka kwa wananchi kila mtu anaenda kusema lake tunaleta mkanganyiko miongoni mwa wananchi. Nafurahi katika Halmashauri yangu nimefanikisha hilo na tupo kitu kimoja.”
Nae Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Abel Suri ameishukuru Halmashauri kwa ukarimu wao na kuwa tayari kuwapatia elimu hiyo kwani imekuaa na manufaa kwao na wamejipanga kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika wakati ujao.
Waliotembelea Halmashauri ya Mji Njombe ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mkurugenzi kamati ya fedha pamoja na wakuu wa idara mbalimbali kutoka Halmashauri ya wilaya ya Ikungi
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe