Ni ziara ya Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo katika Halmashauri ya Mji Njombe ambapo alipata nafasi ya kukagua ujenzi wa kituo cha afya Ihalula na kupongeza shughuli za ujenzi na thamani ya fedha iliyotumika katika ujenzi huo.
“Kwenye ukweli lazima tuseme nimefarijika sana na ujenzi wa kituo hiki mmefanya kazi nzuri nampongeza fundi kwa kazi hii amejenga vizuri sana, licha ya kuwa bado ujenzi huu ungeweza kuwa mzuri zaidi kama usimamizi ungekuwa mzuri kuna makosa madogo madogo yanaonekana kama mhandisi ungekuwa unafanya ukaguzi wa mara kwa mara makosa haya yasingekuwepo usimamizi ni jambo la muhimu katika kazi yoyote ile.”Alisema jafo
Kituo hichi ni miongoni mwa vituo vitakavyotoa huduma za dharura za upasuaji kwa wazazi na utoaji damu salama huku jumla ya Tshs. 500 milioni zikitarajiwa kutumika hadi kukamilika kwake.
Wakati huo huo Waziri jafo alitembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi Mji njombe na kusikitishwa na kusuasua kwa shughuli za ujenzi katika kituo hicho ukilinganisha na Halmashauri ambazo miradi yake ilishakamilika.
Waziri Jafo amemjia juu mkandarasi aliyefanya ujenzi wa awamu ya kwanza na ya pili ambazo zimekamilika kwa kuchelewa sana ambayo ni kampuni ya MASASI CONSTRUCTION na msimamizi wa kituo hicho kwa kuchelewesha ujenzi wa kituo hicho hali iliyopelekea Halmashauri kutafuta Mkandarasi mwingine ambayo ni Kampuni ya HAINAN INTERNATIONAL ambayo imeanza awamu ya tatu ya ujenzi wa kituo hicho na na unataraji kukamilika February 2019 huku kiasi cha shilingi bilioni 5.7 zikitarajiwa kutumika mpaka kumalizika kwake.
“Nisingewaelewa kama Mkandarasi aliyewachelewesha katika ujenzi wa kituo hiki ndio mngekuwa mmempa kazi ya ujenzi wa awamu ya Tatu, Tusingeelewana kabisa. Hatutaki ubabaishaji katika kazi za serikali,wakandarasi wababaishaji hawana nafasi katika awamu serikali hii fedha zipo miradi haiendi msimamizi wa mradi unakuwa huna msaada wowote watu wa aina hii hatuwaitaji wananchi wanahitaji maendeleo. Alisema.
Aidha amemtaka mkandarasi HAINAN INTERNATIONAL kuhakikisha kuwa miezi iliyosalia kazi za uhakika zifanyike na kufikia mwezi agosti yeye mwenyewe atakuja kwa shughuli za uwekaji jiwe la msingi na February Rais afanye uzinduzi wa kituo hicho hivyo wafanye kazi usiku na mchana kwani hakuna muda wa kupoteza tena.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe