Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Mheshimiwa Erasto Mpete Januari 17,2024, ametoa rai kwa watendaji wote ndani ya Halmashauri ya Mji Njombe kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe.Anthony Mtaka kutoa elimu ya lishe bora shuleni na kwenye mikusanyiko ya watu ili kufanikisha kampeni ya kupambana kutokomeza udumavu Mkoani Njombe .
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Shule ya Msingi Nazareth,Mhe.Mpete amewamboa wazazi ,waalimu pamoja na watendaji katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe wakiwemo watendaji kata na viongozi wengine kuhakikisha wazungumza suala la lishe shuleni,kwenye mikutano na maeneo mengine ya mikusanyiko ili kupambana kutokomeza udumavu ndani ya Halmashauri ya Mji Njombe.
“Kwa kuwa Mhe.Mkuu wa Mkoa amefika leo katika shule ya msingi Nazareth basi sisi tujielekeze katika shule nyingine zote zilizopo Halmashauri ya Mji Njombe na tuzungumze mambo haya katika mikusanyiko yote ile iwe ni mikutano iwe ni msiba ili tuweze kuungana na Mkuu wa Mkoa katika suala zima lakutokomeza udumavu “Alisema Mhe.Erasto Mpeta Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Afisa lishe Mkoa wa Njombe Bi Bertha Nyigu na Afisa lishe wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi Fransisca Mosha, wamesisitiza kuwa ustawi mzuri wa mtoto unaanzia kwenye lishe anayopatiwa hivyo ni muhimu kwa akina mama kuzingatia kunyonyesha watoto kama inavyoshauriwa kitaalamu na kuwapa mlo ulio kamili kila siku.
Aidha wamewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wa lishe bora kwenye familia zao kwa kuwaeleza nakuwakumbusha wazazi wao mara kwa mara umuhimu wakuwapatia mlo kamili kila siku.
Mkoa wa Njombe unatajwa kuwa na udumavu kwa kiasi kikubwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.Ni kwa sababu hiyo Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendesha kampeni maalumu ya kutoa elimu ya lishe ili kutokomeza udumavu.
Elimu ya lishe bora inatolewa kwa jamii kupitia vyombo vya habari, kwenye nyumba za ibada , mikutano,shuleni ,vyuoni na maeneo mengine ya mikushanyiko katika Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe