Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe katika Halmashauri, mratibu wa lishe Halmashauri ya Mji Njombe Marselina Mtitu amesema kuwa kwa kipindi cha robo ya tatu Januari – Machi 2021, kitengo cha Lishe kimekuwa kikishughulika na kuboresha hali ya Lishe kwa watoto chini ya Umri wa miaka 5, wanawake wajawazito, wanawake wanaonyonyesha na vijana rika balehe ngazi ya jamii ambapo Kata zilizopatiwa elimu ya utoaji lishe bora kwa kuzingatia makundi matano ya chakula ni Lugenge, Luponde na Uwemba.
Awali akiwasilisha maagizo ya utekelezaji wa kikao kilichopita mratibu huyo amesema kuwa kitengo cha lishe kwa kushirikiana na idara za elimu wamefanikiwa kutembelea katika shule za msingi na kuelimisha juu ya upandaji mbogamboga katika maeneo ya Shule ambapo wamesema kuwa katika Shule zilizotembelewa mwitikio umekuwa ni mkubwa licha ya kuwepo kwa changamoto za maji katika baadhi ya maeneo.
Bi.Mtitu amesema kuwa kwa sasa jamii imeendelea kuelimishwa elimu ya lishe bora kwa kuzingatia makundi matano ya vyakula na kuandaa vipeperushi vya aina ya vyakula katika makundi hayo ili jamii iondokane na ulaji wa lishe isiyozingatia makundi hayo.
Wakitoa maoni yao kwenye kikao hicho baadhi ya wajumbe wamesema kuwa ni vyema elimu juu ya ulishaji wa watoto wachanga na wadogo itolewa katika kila hudhurio la kliniki ili wazazi na walezi waweze kupata uelewa juu ya ulishaji bora.
Kuhusu hali ya utoaji wa matibabu kwa watoto wenye utapiamlo Mtitu amesema kuwa kwa kipindi cha robo ya tatu Januari –Machi 2020/2021 watoto waliotambuliwa ni 46 ambapo kati ya hao watoto 45 walipatiwa matibabu na kuruhusiwa na motto mmoja alipoteza maisha.
Halmashauri ya Mji Njombe imeendelea kufanya jitihada za kupambana na udumavu ambapo sambamba na kufanya vikao vya kujadili utekelezaji wa shughuli za lishe pia Halmashauri imeendelea kutenga bajeti kwa kutumia mapato ya ndani kusaidia shughuli za lishe.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe