Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika leo amekabidhi gari ya kubebea wagonjwa yenye thamani ya shilingi milioni 200 katika kituo kipya cha Afya Kifanya, vyanzo vikuu vya ujenzi wa kituo hicho ikiwa ni mapato ya ndani ya Halmashauri na Nguvu za Wananchi ambapo Wananchi wa Kata ya Kifanya walichangia kiasi cha Shilingi millioni thelathini na nane na laki saba na Halmashauri kupitia mapato ya ndani iliweza kutoa kiasi cha shilingi milioni mia tatu hamsini.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho Mtendaji wa Kijiji cha Kifanya Barick Kabelege amesema kuwa lengo la ujenzi wa Kituo hicho linatokana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuhakikisha kuwa katika kila Kata inatakiwa kuwa na Kituo cha Afya na dhumuni la pili ikiwa ni kutokana na ongezeko la idadi ya watu wanaohitaji huduma za Kiafya katika Zahanati ya sasa ya Muungano ongezeko lililosababishwa na uwepo wa shamba la chai Mahoro na Unilever, shughuli za kibiashara na umbali wa takribani Kilomita 60 kutoka ilipo Hospitali ya Mji Kibena.
“Mpaka sasa tumefanikiwa kujenga majengo 6 ya kiwemo jengo la upasuaji, mortuary, jengo la kufulia jengo la mama na mtoto, maabara na miozi. Tunao pia wachangiaji mbalimbali ambao wamechangia katika kufanikisha ujenzi huu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alituchangia milioni 10, Mbunge aliyepita alichangia mifuko 100 ya saruji, Mheshimiwa Diwani mifuko 50 ya saruji, Umoja wa Wanawake CCM Wilaya ya Njombe mifuko ya saruji 20, Taasisi ta Kifedha Kifanya kiasi cha shilingi laki saba na nusu na CCM Wilaya mifuko 10 ya saruji ambapo kwa pamoja tumekamilisha majengo hayo.”
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo Mbunge wa Jimbo hilo Deo Mwanyika amewashukuru Wananchi wa Kifanya kwa kuitikia wito wa Serikali na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuimarisha Sekta ya Afya katika jimbo hilo jambo lililopelekea Halmashauri hiyo kuwa kati ya Halmasahuri 20 pekee zilizofanikiwa kupata magari hayo nchi nzima.
“Ombi lenu limekua ndio msingi wa ushindi wetu.Ujenzi wa kituo cha afya kifanya ni jambo la kutukuka.Naomba niwahakikishieni kuwa mchango wangu ni kuhakikisha kuwa kituo hiki kinafunguliwa na vifaa tiba vinapatikana. Kwa leo nitawachangia mifuko 100 ya saruji ila yaliyosalia nitakwenda kuyatekelza kwa nguvu zote.Tunamshukuru pia Rais wetu Samia Suluhu Hassani kwani kwa uongozi wake Njombe tutafanya makubwa”Alisema Mwanyika
Aliendelea kusema.”Niwaombe twende tukalitunze gari hili na pia tuhakikishe kuwa tunaitambua na kuilinda mipaka ya kituo chetu ili kuepusha migogoro”Alisema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Njombe Edward Mgaya amewapongeza Wananchi hao na kuwataka kuendeleza utamaduni wa kuchangia kwani licha ya kupatiwa gari lakini kuna wakati mwingine magari hayo yanashindwa kutoa huduma kutokana na kukosekana kwa fedha za mafuta na matengenezo na kuwataka Wabnanchi kuendelea kulihudumia gari hilo ili Wananchi waendelee kupata huduma za msingi
Atilio Mwapinga na Leah Mkalawa wote wakazi wa Kifanya wanasema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kupatia gari hilo kwani kwa sasa walikua wanategemea gari kutoka kituo cha afya mjini takribani kilomita 60 kama akitokea mgonjwa wa rufaa jambo ambalo lilikuwa lilikua linahatarisha maisha ya watu hususani wanawake wajawazito.
Mpaka sasa kituo hicho kipo katika hatua za umaliziaji huku kiasi cha Shilingi milioni mia mbili ishirini na tano kikitarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi huo ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amewahakikishia Wananchi kukamilisha hatua hiyo.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe