Kuelekea siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluh Hassan, Januari 12,2024 Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) Mkoa wa Njombe kwa kushirikina na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, imepanda miti ya mapambo zaidi ya 200 kandokando ya barabara inayoelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe.
Katibu wa JUWAKITA Mkoa wa Njombe Bi. Halima Hamza, amesema wametenga siku hii maalumu kwa kupanda miti ili kumtakia Kheri ya siku ya kuzaliwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluh Hassan, ambaye alizaliwa Januari 27,1960.
Pia ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali inazofanya katika uhifadhi wa Mazingira na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.
Aidha ameeleza kuwa zoezi la upandaji miti kwa Jumuiya hiyo litakuwa endelevu na wataendelea kuhamasisha wanawake wengine na jamii kwa ujumla kupanda miti hasa wakati huu wa mvua.
Kwa upande wake Katibu wa JUWAKITA Wilaya ya Njombe Zaituni Mahimbo, amesema miti waliyoipanda ni sadaka na ni alama ya kumbukumbu kwa wanafunzi walioshiriki kupanda miti hiyo na vizazi vijavyo vitakavyoishi Mkoani Njombe.
Naye Afisa Maliasili wa Halmashauri ya Mji Njombe John Sanga ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Njombe kwenye tukio hilo, amewapongeza wanawake wa Jumuiya hiyo Mkoani Njombe kwa kuamua kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluh Hassan kwa kupanda miti ambayo ni kumbukumbu ya kudumu.
Sanga amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamashisha zoezi la upandaji wa miti na kwa mwaka huu Halmashauri ya Mji kwa kushirikina na wadau imezalisha miche ya miti aina tofauti milioni 13 ambayo itapandwa kwenye maeneo tofauti tofauti ndani ya Halmashauri.
Aidha ametoa wito kwa jamii kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuacha kuchoma misitu na kukata miti kwenye vyanzo vya Maji.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe