Ni mapendekezo yaliyotolewa katika Baraza Maalumu la kujadili hoja za mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali CAG katika Halmashauri ya Mji Njombe ambapo kwa mwaka 2019/2020 kiasi cha Shilingi Milioni 42.8 kinadaiwa kutoka kwenye madeni ya vikundi vya Wanawake na Vijana ambapo Madiwani wameitaka Kamati ya Maendeleo ya Kata (KAMAKA) kushiriki katika kuhakiki vikundi vitakavyopatiwa mikopo ili kujiridhisha.
Akichangia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya fedha baadhi ya Waheshimiwa Madiwani Edwin Mwanzinga Diwani wa Kata ya Matola,Filoteus Mligo Diwani wa Kata ya Lugenge na Diwani Viti Maalumu Njombe Mjini Tumaini Mtewa wamesema kuwa ni vyema vikundi hivyo vikaendelea kufuatiliwa kwa karibu zaidi ili wakopaji waweze kurejesha fedha hizo na hoja ziweze kufungwa kwa wakati na pia utaratibu wa Kuwahusisha Kamati ya Maendeleo ya Kata ukafuatwa ili ufuatiliaji uwe wa ukaribu.
“Kwenye utoaji Mikopo usipotoa mikopo ni hoja. Ukitoa mikopo wasiporejesha ni hoja. Napendekeza majina ya vikundi yapitishwe kwenye KAMAKA ili tuweze kujua ni vikundi gani vinavyokopa kwenye Kata hata ufuatiliaji utakuwa rahisi. Kwenye kurejesha pia tutakamatana Madiwani humu ndani kwani sisi ndio Wenyeviti wa KAMAKA. Hii itasaidia katika kufanya marejesho kwa wakati kwa vikundi” Alisema Mwanzinga Diwani wa Kata ya Matola.
“Ukiangalia katika vikundi vinavyodaiwa wengi wanatoka katika Kata za Njombe Mjini,Ramadhani na Mjimwema. Maeneo ya Mjini wamekuwa wasumbufu katika urejeshaji wa mikopo.Ni vyema sasa katika vipindi vijavyo fedha hizi tukatoa kwa Kata zinazorejesha “Alisema Diwani wa Kata ya Makowo Honolatus Mgaya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya ametoa muda wa miezi mitatu kuhakikisha kuwa kiasi cha Shilingi milioni 42.8 za marejesho ya vikundi zinarejeshwa ili ziweze kuwanufaisha walengwa katika maeneo mengine na ametoa miezi mingine mitatu kuhakikisha kuwa makusanyo ya shilingi milioni 61.3 ya waliokuwa mawakala wa ukusanyaji mapato ya Halmashauri yanarejeshwa kwa Halmashauri
“Tunaovijana waliomaliza mafunzo ya jeshi la kujenga taifa. Wengi hawajafanikiwa kupata ajira zilizo rasmi na wanataaluma mbalimbali. Tunaweza kuwaweka kwenye vikundi kwa kadri ya taaluma zao na kuwapatia mikopo ambayo itawasaidi katika kupata ajira stahiki” Alisema Rubirya.
Licha ya kuipongeza Halmashauri kwa ushirikiano kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupata hati safi pia ameitaka Halmashauri kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuendelea kusimamia utoaji wa huduma na kuipongeza kwa hatua ambayo Halmashauri imeanza kuchukua ya kuipandisha hadhi kutoka kuwa Mji kwenda kwenye Manispaa.
Kwa mwaka 2019/2020 katika miamala ya hesabu za mwisho Halmasahuri ilipata hati inayoridhisasha (Safi) ambapo Halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 38 kati ya hizo 19 zikiwa ni hoja za nyuma na 19 zikiwa ni hoja za mwaka husika.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe