Wajumbe wa Kamati ya kudumu Bunge inayojihusisha na UKIMWI imefanya ziara katika Mkoa wa Njombe ambapo imepokea taarifa ya hali ya maambukizi Mkoa,Kukagua shughuli za kiuchumi zinazofanywa na walengwa,kutembelea kituo cha kutolea dawa na ushauri CTC kilichopo katika Hospitali ya Mkoa Wikichi na kutembelea Magereza ambapo kamati hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake Fatma Tawfiq imeshauri elimu zaidi kwa jamii kuepuka maambukizi mapya ikiwa sambamba na matumizi ya mipira ya kike na kiume.
Akisoma taarifa ya hali ya maambukizi hayo, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Robert Masele ambaye ni mratibu wa Ukimwi Mkoa huo, amesema hali ya maambukizi katika Mkoa imepungua kutoka asilimia 14.8 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 11.4 mwaka 2017 ambapo Mkoa umeendelea kuweka mikakati thabiti ili kuhakikisha kuwa hakuna kasi ya maambukizi mapya huku jamii ikiendelea kuhamasishwa kujitokeza kupima afya zao.
Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Marwa Rubirya alisema taarifa ya hali ya tohara katika Mkoa huo ilikuwa chini kwa miaka mingi kutokana na tamaduni, mila na desturi za wakazi wa Njombe na hivyo kuongeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi katika maeneo mengi ambapo Mwenyekiti wa hiyo, Mhe. Fatma Tawfiq, amewataka watendaji wa Mkoa huo waongeze juhudi katika kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na matumizi ya kondomu pamoja na kuhamasisha tohara kwa wanaume.
Kwa upande wake Naibu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Godwin Mollel akichangia katika kikao hicho, amesema kuwa Wizara imekuja na mfumo rasmi ambapo mfumo huo utatumika kwa ajili ya kuzisajili Asasi zisizo za Kiserikali (NGO) zinazoratibu masuala mbalimbali ikiwemo UKIMWI jambo ambalo litapeleka Mkoa kutambua shughuli halisi na maeneo Asasi hizo zinapofanya kazi jambo litakalopelekea kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Halmashauri ya Mji wa Njombe inakadiriwa kuwa na takribani watu 22,537 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na Wilaya nyingine zilizomo katika Mkoa huo.
Katika ziara hiyo Kamati hiyo pia iliweza kukagua Ofisi ya Baraza la watu wanoishi na Maambukizi katika Halmashauri ya Mji Njombe (KONGA) ambapo wamefarijika kwa kuona hatua ambazo Halmashauri imeweza kuchukua ikiwa ni pamoja na kuwasaidi wanufaika hao katika shughuli zao za kuwaingizia kipato.
Aidha wamemtaka Mkurugenzi kuendelea kusaidi kundi hilo kwani linamchango mkubwa katika kuinua uchumi wa familia zao na uchumi wa nchi kwa ujumla kutokana na shughuli za kijasiriamali zinazofanywa na walengwa hao.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe