Halmashauri ya Mji Njombe imetoa mafunzo kwa Madiwani, Watendaji wa Kata, Waratibu Elimu, Maafisa Tarafa na Wakuu wa Shule za Sekondari lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo wa namna ya kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Mafunzo hayo yanafuatia ziara iliyofanywa na Kamati ya Fedha na Utawala kwenye ukaguzi wa miradi ambapo ilibaini uwepo wa changamoto katika usimamizi wa ujenzi katika sekta ya afya na elimu. Mafunzo hayo yaliambatana na uandaaji wa mipango mikakati ya ukusanyaji mapato.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Bi Illuminatha Mwenda alisema kuwa Halmashauri ya Mji Njombe kwa mwaka wa fedha uliopita zaidi ya Shilingi bilioni moja zilipelekwa kwenye Kata kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo na hivyo kuona ni vyema kuwapatia elimu ya usimamizi wa miradi hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Njombe Edwin Mwanzinga amesema kuwa zipo baadhi ya Kata ambazo zimekuwa hazizingatii kanuni na taratibu katika usimamizi wa miradi na manunuzi jambo ambalo limekuwa likileta migogoro na kuibua hoja zisizo za lazima jambo ambalo amekemea na kuzitaka Kamati hizo kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia kanuni na taratibu.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo hayo wamesema kuwa elimu waliyoipata imekua na manufaa makubwa na kuahidi kuitumia vyema katika kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na ubora uliokusudiwa.
Mada zilizotolewa ni pamoja na usimamizi wa sheria za manunuzi ,wajibu wa Waheshimiwa Madiwani katika kusimamia miradi ya maendeleo,utaratibu wa kuingia mikataba,jitihada za jamii,usafi wa mazingira mapato na matumizi ya mifumo katika kukusanya mapato.
Ofisi yetu inapatikana barabara ya Njombe-Songea mtaa wa Mjimwema.
Sanduku la Posta: S.L.P 577
Simu ya Mezani: 026-2968833
Simu ya Mkononi: 026-2968833
Barua Pepe: td@njombetc.go.tz
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Mji Njombe